36. Kubwa ambalo Allaah amewaamrisha waja ni Tawhiyd

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kubwa Aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah.

MAELEZO

Kubwa aliloamrisha… – Hili ni jambo muhimu mno. Hakika Tawhiyd ndio kubwa aliloamrisha Allaah. Maamrisho yote yaliyoamrishwa na Allaah yanakuja baada ya Tawhiyd. Ni ipi dalili inayoonyesha kwamba kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd? Amesema (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote… ”[1]

Ndani ya Aayah hii mna haki kumi. Kwa ajili hiyo inaitwa Aayah ya haki kumi. Ya kwanza katika haki hizi ni haki ya Allaah (Subhaanah):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote na watendeeni wema wazazi wawili… “

Hii ndio haki ya pili.

وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ

“… na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa wa karibu.”

Hii ni haki ya tatu. Jamaa wa karibu ni wale ambao mmekutanisha ujamaa wa kinasaba kupitia kwa baba au kwa mama kama mfano wa kina baba wakubwa na wadogo, mababu, mashangazi, wajomba, kina mama wakubwa na wadogo, kina kaka, kina dada, watoto wa kaka yako na watoto wa dada yako na mabinamu. Hawa ndio jamaa wa karibu. Wana haki ya udugu.

وَالْيَتَامَىٰ

“… na mayatima.”

Mayatima miongoni mwa waislamu. Ni kila yule ambaye amefiwa na baba yake akiwa bado ni mdogo hajabaleghe na akawa ni mwenye haja ya mwenye kuziba pengo la baba yake katika kumwangalia mtoto huyu kimalezi, kumhudumikia, kumtekelezea mahitajio yake na kumwondoshea yenye kumdhuru. Kwani hana baba wa kumlinda, kumpa matumizi na kumtetea. Kwa hiyo yuko na haja ya mwenye kumsaidia. Kwa sababu amempoteza baba yake na familia yake. Yuko na haki katika Uislamu.

Muhimu ni kwamba Allaah amezianza kwa haki Yake pale aliposema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote… ”

Hakufupika kusema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ

“Na mwabuduni Allaah.”

Kwa sababu ´ibaadah haisihi na wala hainufaishi pamoja na shirki. Haiitwi ´´ibaadah` isipokuwa pale inapokuwa imefanywa kwa ajili ya Allaah pekee. Ikiwa iko pamoja na shirki haiwi ni ´ibaadah vovyote mja atavyoichokesha nafsi yake kwayo. Amri ya jambo la ´ibaadah imeambatana na makatazo ya shirki. Kwani ´ibaadah haisihi muda wa kuwa bado shirki ipo. Hii ni dalili ya maneno ya Shaykh:

“Kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd.”

Kwa vile Allaah ameanza kwayo katika Aayah nyingi kukiwemo Aayah hii pia. Miongoni mwazo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”

Ameanza (Subhaanah) kwa Tawhiyd. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa ndio kubwa ambalo Allaah ameamrisha:

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ

”Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Mola wenu kwenu kwamba: “Msimshirikishe na chochote; na muwafanyie wema wazazi wawili; na wala msiwaue watoto wenu kutokana na umasikini.”[2]

Hii ni dalili juu ya yale yatayokuja huko mbele kwamba kubwa alichokataza Allaah ni shirki.

Ikiwa kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd basi ni lazima kwa mtu kuanza kujifunza ´Aqiydah kabla ya kila kitu kingine. ´Aqiydah ndio msingi. Hivyo ni lazima kwa mtu kuanza nayo wakati wa kujifunza na kuifunza na adumu kuifunza na kuibainisha. Kwani ndio kubwa aliloamrisha Allaah. Si jambo munasibu kuifanya ndio kitu cha mwisho au mtu asiipe uzito wowote. Kwa sababu hii leo wapo walinganizi wanaopuuza kuifunza Tawhiyd na ´Aqiydah. Wapo watu waliopewa mtihani huo. Jengine ni kwa sababu kuiharibu ni kuharibu dini yote. Kwa hivyo ni lazima kuitilia umuhimu.

[1] 04:36

[2] 06:169

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 10/12/2020