35. Vipande viwili vyembamba vya mkate na maji

191 – Daawuud bin ´Amr adh-Dhwabbiy ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar, ameeleza kuwa ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia wafuasi na wafuasi zake:

”Lazimianeni na mkate wa shayiri, uleni na chumvi kidogo na wala msiule isipokuwa pale mnapoutamani. Vaeni nguo zilizotengenezwa kwa nywele, hivyo muiache dunia hali ya kuwa mmesalimika. Nawaambia kwa haki kabisa ya kwamba utamu wa dunia ni uchungu wa Aakhirah na hakika uchungu wa dunia ni utamu wa Aakhirah. Hakika waja wa Allaah hawaishi maisha ya kifahari. Nawaambieni kwa haki kabisa ya kwamba muovu wenu zaidi anayetenda ni mwanazuoni anayeipenda dunia na akaipa kipaumbele juu ya elimu yake. Lau angeliweza, basi angeliwafanya watu wote wafanye kama yeye.”

192 – al-´Abbaas bin Ja´far ametuhadithia: Muslim bin Ibraahiym ametuhadithia: Abaan ametuhadithia: Qataadah ametuhadithia: Anas ametuhadithia:

”Chakula cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si cha mchana wala cha jioni hakikuweza kuwa na nyama na mkate, isipokuwa kama kuna mkusanyiko wa watu.”[1]

193 – Abu ´Aliy al-Marwaziy ametuhadithia: ´Abdaan bin ´Uthmaan ametuhadithia: ´Abdullaah ametukhabarisha: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametukhabarisha: Shurahbiyl bin Muslim ametuhadithia:

”´Amr bin al-Aswad al-´Ansiy mara nyingi alikuwa akiacha kule kushiba kwa sababu ya kuchelea kiburi.”

194 – Muhammad bin al-Husayn amenihadithia: ´Ubaydullaah bin Muhammad at-Taymiy ametuhadithia: Muhammad bin Mis´ar amenihadithia, kutoka kwa baadhi ya wanamme wake, ambao wamesema:

”Tumefikiwa na khabari kwamba njaa ya kitambo kirefu inapelekea hekima.”

195 – Muhammad amesema: Yahyaa bin Ishaaq ametuhadithia: Hishaam bin Laahiq ametuhadithia, kutoka kwa bwana mmoja kutoka Swan´aa’, kutoka kwa Wahb bin Munabbih, ambaye amesema:

”Njaa ni busara ya mwili; inausafisha na kuulainisha.”

196 – Muhammad amesema: Qudaamah bin Muhammad ametuhadithia, kutoka kwa Makhramah bin Bukayr bin ´Abdillaah bin al-Ashajj, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Ilikuwa inasemwa kwamba mtu asilifanye tumbo lake likajazwa na vitu visivyostahiki. Linatoshelezwa na tende, matonge kadhaa na kitu kidogo.”

197 – Muhammad amesema: Bishr bin ´Umar az-Zahraaniy ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Sulaymaan, ambaye ameeleza:

”Bwana mmoja alisema kumwambia Maalik bin Diynaar: ”Ee Abu Yahyaa, inakutosha mikate miwili ya bata kwa siku?” Akajibu: ”Hivyo nitakuwa nataka kuwa mnene. Vipande viwili vyembamba vya mkate na maji; ni vyakula vinavyomtosha muumini mpaka wakati wa kufa kwake.”

198 – Muhammad ametuhadithia: al-´Abbaas bin al-Fadhwl al-Azraq ametuhadithia: Abu Sa´iyd ametuhadithia: Nimemsikia al-Hasan akisema:

”Naapa kwa Allaah! Yote ni kwa ajili tu ya kueshi. Muumini hana chochote katika starehe za maisha ya kidunia.”

199 – Muhammad amesema: as-Swalt bin Hakiym ametuhadithia: Nimemsikia ´Abdullaah bin Marzuuq akisema:

”Sioni kama kuna yeyote, ambaye moyoni mwake kuna chembe kidogo ya kuipenda dunia, kuwa anafikia ngazi ya njaa.”

[1] Ahmad (3/270).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 124-128
  • Imechapishwa: 30/07/2023