Allaah amrehemu kiongozi wa Waumini ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz pindi aliposema:

“Iridhie nafsi yako yale yaliyoridhiwa na watu juu ya nafsi zao. Walisimama kutokana na elimu na utambuzi. Kungelikuwa kuna kheri yoyote ndani yake basi wangeigundua na kuifuata kabla yenu. Wao ndio wa mwanzo waliotangulia. Ikiwa uongofu ni yale mliyomo nyinyi, basi wangekutangulieni. Na kama ni kitu kipya kilichozuliwa baada yao, basi hakikuzuliwa isipokuwa na ambao wanafuata njia isiyokuwa yao na wakawapa mgongo. Wamesema yenye kutosheleza na yenye kukidhi haja. Yote yaliyo chini yao ni ya upungufu na yote yaliyo juu yao ni uchoshi. Baadhi walipuuza njia yao wakazembea, wengine wakaingiwa na tamaa ambapo wakachupa mipaka. Wako kati ya hayo, katika njia ilionyooka.”[1]

´Allaamah na Shaykh ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan Abaa Butwayn (Rahimahu Allaah) alipokuwa anaraddi baadhi ya mambo yaliyozuliwa:

“Kama yangelikuwa mazuri na yenye kupendeza kwa Allaah, basi wangetutangulia kwayo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walisimama baada yao. Wao wenyewe walikuwa wakisema:

“Fuateni na wala msizue. Hakika mmetoshelezwa. Kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Walikuwa (Radhiya Allaahu ´anhum) ni wajuzi zaidi na wenye kupupia zaidi mambo ya kheri. Yule ambaye atazua kitu anachojikurubisha kwacho mbele ya Allaah ambacho si Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakukifanya kuwa ni ´ibaadah, basi hakika ameweka kitu katika Shari´ah ambacho hakikuidhinishwa na Allaah:

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyatolea kwayo idhini?”[3]

Isitoshe anawakosoa Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya kwamba amejua kitu ambacho wao hawakukijua, au kwamba hawakutendea kazi kitu walichokijua. Hilo linapelekea kuwatia wale wa mwanzo waliotangulia ambao ni wahamiaji na wanusuraji, ima ujingani au upungufu katika matendo. Wao (Radhiya Allaahu ´anhum) kama tulivotangulia walisimama baada yao. Kheri yote inapatikana kwa kule kuwafuata na shari yote inapatikana kwa kuzua.”[4]

[1] Abu Daawuud (5/19), Ibn Wadhdhwaah katika ”al-Bid´a wan-Nahiy ´anhaa”, uk, 30, al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah”, uk. 233, na Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (5/337).

[2] Wakiy´ katika ”az-Zuhd” (315), Ahmad (3/110), Ibn Wadhdhwaah (13), Ibn Naswr (81), at-Twabaraaniy (8770) na ad-Daarimiy (211).

[3] 42:21

[4] ad-Durar as-Saniyyah (8/106).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 17/05/2023