Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Enyi watu! Hakika mtakuja kuzusha na mtakuja kuzushiwa. Mtakapoona kilichozuliwa, basi lazimianeni na lile jambo la kwanza.”[1]

Amesema tena akiwausia wanamme na wanawake:

“Yule mwanamke au mwanamme atakayeishi kipindi kirefu basi alazimiane na ile njia ya kwanza – njia ya kwanza!”[2]

Amesema tena:

“Tafuteni elimu kabla haijapotea. Inapotea kwa kuondoka kwa wanazuoni. Mtawapata watu wanaodai kuwa wanalingania katika Kitabu cha Allaah, ilihali ukweli wa mambo wamekitupa nyuma ya migongo yao. Kwa ajili hiyo tafuteni elimu na jiepusheni mbali na Bid´ah. Jiepusheni mbali na mambo ya kujikakama na kuingia kina na lazimianeni na jambo la kale.”[3]

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Enyi wanazuoni! Ifuateni njia yetu! Naapa kwa Allaah mkitufuata, basi hakika mtakuwa mmetangulia mbali kabisa. Na mkiiacha na mkaamua kushika njia ya kuliani na kushotoni, basi hakika mtakuwa mmepotea upotevu wa mbali kabisa.”[4]

Mapokezi haya yanahamasisha kufuata njia ya Maswahabah wakati wa kukithiri Bid´ah na mambo yaliyozuliwa. Hayo yanapatikana katika maneno ya Ibn Mas´uud na Hudhayfah “…lazimianeni na jambo la kale” na “Ifuateni njia yetu!” Wakati mazingira yamechafuliwa kwa uchafu wa matamanio na uzushi, basi uokozi unapatikana kwa kushikamana barabara na njia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Yapime maneno na matendo yote kwa maneno na matendo yao. Yale yanayoafikiana na maneno na matendo yao ndio yenye kukubaliwa, na yaliyo kinyume na hivyo ni yenye kurudishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipokuwa akisifia kundi Lililookokaa:

“Mayahudi wamegawanyika mapote sabini na moja. Manaswara wamegawanyika mapote sabini na mbili. Na Ummah huu utagawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Wakasema: “Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile linalofuata yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[5]

[1] ad-Daarimiy (1/56).

[2] ad-Daarimiy (1/63).

[3] al-Bayhaqiy katika ”al-Madkhal” (388).

[4] Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih (2/97).

[5] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 41
  • Imechapishwa: 17/05/2023