36. Si kila mtu ana uwezo wa kufanya Ijtihaad yake

Kuna uzindushi muhimu unaohusiana na manufaa yaliyoachiwa (المصالح المرسلة) na ambalo wameghafilika nalo wengi katika wale watetezi wake. Lau wangezingatia nukta hii, basi jambo lisingekuwa na vuguru kama ilivyo hii leo. Nukta yenyewe ni kwamba ni vigumu kuweka kikomo cha manufaa katika jambo fulani. Mtazamaji anaweza kufikiri kuwa kitu fulani ni manufaa lakini mambo yakawa sivo hivyo. Kwa ajili hiyo wanazuoni pekee na wenye upeo wa kufanya Ijtihaad na ambao wako na uadilifu na uoni wa mbali juu ya hukumu za Shari´ah na manufaa ya kilimwengu ndio wanaostahiki kuamua ni kipi chenye manufaa yaliyoachiwa. Kwa sababu uwezo huo unahitaji “hadhari ya hali ya juu na uangalifu mkubwa wa kuzidiwa na matamanio. Mara nyingi matamanio huyapambia madhara ambapo yakayaona ni manufaa, na mara nyingi hudanganyika kwa mambo ambayo madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake”[1]. Shaykh ´Umar al-Faasiy amehakikisha maana kama hiyopale aliposema katika “al-Waqf”:

“Ni vipi mtu anayefuata kichwa mchunga atadai dhana kubwa kwamba manufaa haya yanafikia malengo ya dini na kwamba hakuna katika dini kinachopingana nayo wala kitu kinachojulisha kutosihi kwake? Ijapokuwa hakufanya utafiti kwenye dalili wala hakutafiti yaliyomo ndani yake. Ni kitu gani hiki kama sio kuwa na ujasiri juu ya dini na kuiparamia hukumu ya Shari´ah pasi na yakini?”[2]

Nimetaja jambo hili ili wale watu wenye papara wanaopekua manufaa yaliyoachiwa watambue namna ilivyo vigumu njia waliyoamua kushika. Hebu wawaachie njia hiyo wenye nayo wanaostahiki.

Mpaka hapa tutakuwa tumemaliza maoni ya kwanza yanayosema kulingania hakuhitajii kuwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Huko mbeleni tutataja baadhi ya hoja za maoni hayo pamoja na kuziraddi.

[1] Maswaadir-ut-Tashriy´ al-Islaamiy, uk. 85

[2] Tazama ”´Ilm Usuul-il-Bid´ah”, uk. 235 ya ´Aliy bin Hasan al-Halabiy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 17/05/2023