´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Wakati Sa´d bin ´Ubaadah alipoumwa, alikuja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtembelea akiwa pamoja na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Sa´d bin Abî Waqqaas na ´Abdullaah bin Mas´uud. Walipoingia kwake wakamkuta amepoteza fahamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Amekwishaaga dunia?” Wakasema: “Hapana, ee Mtume wa Allaah.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kulia. Pindi watu walipoona jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analia nao pia wakaanza kulia. Ndipo akasema: “Hamsikii? Hakika Allaah haadhibu kwa macho kutiririka machozi wala moyo kuhuzunika. Lakini anaadhibu kwa hiki” na akaashiria kwenye ulimi wake.”[1]

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“ Tuliingia pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Abu Sayf al-Qayn, ambaye alikuwa ameolewa na mama yake Ibraahiym wa kunyonya. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamchukua Ibraahiym, akambusu na kumnusa. Baada ya hapo na sisi tukaingia. Ibraahiym alikuwa katika hali ya kukata roho. Macho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yakawa yanatiririka machozi. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) akamwambia: “Na wewe pia, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ee mwana wa ´Awf, hii ni huruma!” Kisha akafuatisha jengine, kisha akasema:  “Hakika macho hutokwa na machozi, moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”[2]

Salamah bin Muhaarib amesema:

“Wakati Ibraahiym, mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alipokuwa katika hali ya kukata roho, aliwekwa katika mapaja ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Lau isingelikuwa miadi ya kweli na ahadi iliyokusanya na kwamba yule mwenye kutangulia anawakilishwa na aliyebakia na kwamba yule wa mwisho atakuja kuungana na yule wa kwanza, basi ningekuhuzunikia, ee Ibraahiym.” Macho yake yakatokwa na machozi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Macho yanatokwa na machozi, moyo unahuzunika na wala hatusemi isipokuwa yale yanayomridhisha Mola (´Azza wa Jall). Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”

az-Zubayr bin Bakkaar amepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin Muhammad bin ´Umar bin ´Aliy bin Abiy Twaalib, ambaye ameeleza:

“Baada ya Ibraahiym, mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufa, akatoka (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) naye na akawa anatembea mbele ya machela yake. Kisha akaketi karibu na kaburi lake. Halafu akateremka ndani ya kaburi lake. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona amewekwa ndani ya kaburi lake, macho yake yakatokwa na machozi. Pindi Maswahabah walipoona jambo hilo wakaanza kulia mpaka sauti zao zikawa juu. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akamwelekea na kusema: “Ee Mtume wa Allaah, unalia ilihali wewe unakataza kulia?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “ Ee Abu Bakr! Macho hutokwa na machozi, moyo ukaumia na wala hatusemi yanayomchukiza Mola.”[3]

Imepokelewa kuwa Sulaymaan bin ´Abdil-Malik wakati alipofariki mwanawe Ayyuub, alisema kumwambia ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz na Rajaa’ bin Haywah:

“Hakika mimi nahisi kwenye ini langu maumivu ambayo hayawezi kupozwa isipokuwa tu na mawaidha.” ´Umar akasema: “Mtaje Allaah, ee kiongozi wa Waumini, lazimiana na subira!”Akamtazama Rajaa’ bin Haywah ili kumuonyesha kuwa ushauri wake ulikuwa wenye kutuliza. Rajaa´ akasema: “Yatekeleze, ee kiongozi wa Waumini! Haidhuru. Baada ya kuaga dunia Ibraahiym mtoto wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), macho yake yalitokwa na machozi na akasema: “Hakika macho hutokwa na machozi, moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.” Sulaymaan akainamisha macho yake na akalia mpaka akamaliza huzuni yake. Baada ya hapo akawaelekea na kusema: ”Kama nisingepata mawaidha haya, basi huzuni yangu ingelizidi kubwa na kubwa.” Baada ya hapo hakulia tena. Baada ya kumzika mwanawe Ayyuub na akaweka udongo juu ya kaburi lake, alisema: ”Ee kijana, kipando cha mnyama wangu!” Kisha akalielekea kaburi lake na kusema:

Nimesimama kwenye kaburi la kudumu katika ardhi isiyo na kitu –

ilikuwa ni starehe ya muda mfupi kwa kipenzi aliyetengana

[1] al-Bukhaariy (1304) na Muslim (924).

[2] al-Bukhaariy (1303) na Muslim (2315).

[3] Muntakhab min Kitaabi Azwaaj-in-Nabiy, uk. 72-73, ya Ibn Zabaalah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 119-125
  • Imechapishwa: 28/08/2023