34. Chakula alichozowea kula ´Umar bin al-Khattwaab

185 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid ametukhabarisha, kutoka kwa Musw´ab bin Sa´d, ambaye amesimulia:

”Hafswah bint ´Umar alimwambia ´Umar: ”Ee Kiongozi wa waumini! Lau ungelivaa laini zaidi kuliko unazovaa na ukala chakula laini zaidi kuliko unachokula. Kwani Allaah amekufungulia ardhi na akakufanyia kheri kuwa nyingi.” Akasema: ”Hebu wacha nikuhukumu kwa nafsi yangu; wewe hukumbuki jinsi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikumbana na shida za maisha?” Akaendelea kumkumbusha mpaka akamliza. Kisha akasema: ”Mimi nimeshakwambia naapa kwa Allaah najaribu kuishi maisha magumu kama wawili hao, pengine nataraji tukapata maisha ya starehe.”

186 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Ja´far bin Sulaymaan ametukhabarisha, kutoka kwa Hishaam, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”´Umar bin al-Khattwaab hakula isipokuwa kilichochanganywa na shayiri mpaka alipoaga dunia. Wakati mwingine tumbo lake linanguruma, hulipiga kwa mkono wake na akasema: ”Subiri! Naapa kwa Allaah! Mimi sina isipokuwa kile unachokiona mpaka pale utapokutana na Allaah.”

187 – Ishaaq ametuhadithia: Muhammad bin Jaabir ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Shammar bin ´Atwiyyah, kutoka kwa Yahyaa bin Wathaab, ambaye amesema:

”´Umar alimwamrisha mtumwa wake mmoja amfanyie uji wa ngano na akasema: ”Ipike mpaka iondoke ile nguvu ya mafuta. Kuna watu waliojiharakishia mazuri yao katika maisha yao ya dunia.”

188 – Ishaaq ametuhadithia: Ibn ´Ulayyah ametukhabarisha, kutoka kwa Yuunus bin ´Ubayd, kutoka kwa Humayd bin Hilaal, ambaye amesimulia kuwa att ´Umar amesema:

”Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Kama sio kuchelea kupungua kwa mema yangu, basi ningeshirikiana nanyi katika starehe ya maisha yenu.”

189 – Muhammad bin al-Husayn amesema: Ismaa´iyl bin Ziyaad ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Thaabit al-´Abdiy, kutoka kwa Abu ´Imraan al-Juuniy, ambaye amesimulia kwamba ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

”Sisi tuna ujuzi wa chakula kizuri kuliko wengi wanaokila, lakini tunakiacha kwa ajili:

يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا

”Siku mtakapoiona, kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake.”[1]

Abu ´Imraan amesema: ”Naapa kwa Allaah! Yeye pamoja na familia yake walikuwa wakila vya kutosha kwa ajili tu ya kuweza kueshi.”

190 – Surayj amenihadithia: Hushaym ametuhadithia: ´Awf ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”´Umar aliingia nyumbani kwa mwanawe na akamkuta yuko na nyama safi. Akasema: ”Nini hii?” Akasema: ”Tumetamani nyama, hivyo tukanunua kwa dirhamu moja.” Akasema: ”Je, utakuwa unanunua nyama kila unapoitamani? Inatosha kwa mtu kufanya ubadhirifu kula kila anachokitamani.”

[1] 22:2

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 121-123
  • Imechapishwa: 26/07/2023