32. Mifumo ndani ya Qur-aan na Sunnah ni yenye kutosheleza

Yakitambulika yaliyotangulia, basi tunarudi katika ile tafsiri kuitengua kwa yale aliyothibitisha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika fatwa yake ndefu ambayo anabainisha kuwa Shari´ah haikupuuza njia yoyote ya ulinganizi ambayo Allaah anawaongoza kwayo wapotofu. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Yakishatambulika hayo, basi inajulikana kuwa Allaah anawaongoza wapotofu, anawaelekeza waliopotoka na anawasamehe watenda maasi kupitia Kitabu na Sunnah alivyomtumia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vinginevyo, endapo vile ambavyo Allaah amemtumia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) havitoshelezi katika jambo hilo, basi ingelikuwa dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni pungufu na inahitaji kukamilishwa. Mtu anapaswa kujua kuwa Allaah ameamrisha matendo mema, ima kwa njia ya ulazima au ya mapendekezo, na amekataza matendo maovu. Kitendo kikikusanya manufaa na madhara, basi ni hekima ya Mwekaji Shari´ah; manufaa yake yakishinda madhara yake, kitendo kinakuwa kimewekwa katika Shari´ah, na madhara yake yakishinda manufaa yake, kitendo hakikuwekwa katika Shari´ah – bali kinakuwa chenye kukatazwa.

Pindi watu wanapoona kitendo fulani kinawakurubisha kwa Allaah, lakini hakikuwekwa katika Shari´ah na Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ni lazima madhara yake yashinde manufaa yake. Mwekaji Shari´ah asingekipuuza iwapo manufaa yake yanashinda madhara yake. Kwani yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mwenye hekima na hapuuzi yale mambo yenye manufaa katika dini na wala hawakoseshi waumini yale mambo yanayowasogeza mbele ya Mola wa walimwengu… kwa ajili hiyo haijuzu kusema kuwa Allaah hakumtumiliza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia zilizosuniwa zinazowafanya watenda maasi kutubia. Hakika inatambulika kilazima na kupitia nukuu zilizopokelewa kwa mapokezi mengi ambazo Allaah (Ta´ala) pekee ndiye anayejua ni nyumati ngapi zilizotubia kutokamana na kufuru, maasi na makosa kupitia njia zilizowekwa katika Shari´ah.”

Mambo yakishakuwa hivo, na ndivo yalivyo, mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini mlinganizi aende katika njia ambazo hazikuwekwa katika Shari´ah. Yale yaliyotajwa katika Shari´ah yanatosha kuweza kufikia malengo ya kulingania kwa Allaah (Ta´ala), nayo ni kuwafanya watenda maasi kutubia na kuwaongoza wapotevu.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 16/05/2023