31. Uislamu hauyapuuzi manufaa ya waja

Hapa kunajitokeza swali ambalo linahitajia majibu, nalo ni: Je, Shari´ah inapuuza manufaa ya waja? Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amejibu swali hilo wakati alipokuwa anazungumzia manufaa yaliyoachiwa na makinzano juu yake ambapo akasema:

“Maoni yanayosema manufaa yaliyoachiwa mara nyingi yanaweka katika Shari´ah yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha.”

Amesema (Rahimahu Allaah) tena:

“Kwa kufupisha ni kwamba Shari´ah haipuuzi manufaa moja kwa moja. Bali Allaah (Ta´ala) ametukamilishia dini na akatutimizia neema. Hakuna chochote kinachotukurubisha na Pepo, isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuzungumzia nacho. Ametuacha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika weupe; usiku wake ni kama mchana wake. Hakuna anayepotea isipokuwa yule anayestahiki maangamivu.

Mtu mwenye busara akiona kitu ni chenye manufaa na hakikutajwa katika Shari´ah, basi ima Shari´ahimelifahamisha hilo pasi na mwenye kutafakari huyu kuliona hilo, au pia sio manufaa ijapo huyu mwenye kutafakari ataona kuwa ni manufaa. Kwa sababu maslahi ni yale manufaa ya wazi au yenye nguvu zaidi. Mara nyingi watu hufikiri kuwa jambo fulani ni lenye manufaa katika dini na dunia lakini manufaa yake yakawa yamezidiwa nguvu na madhara.”[1]

Hili halipelekei kupinga msingi wa manufaa yaliyoachiwa. Bali ni jambo la haki, lakini halifanyiwi kazi isipokuwa wakati wa kutimia vigezo vyake vilivyotajwa na wanazuoni. Mwenye kutafakari akishikamana na vigezo hivi, ataona kuwa manufaa yaliyoachiwa “yana msingi katika dalili za  Shari´ah”[2]. Kukusanywa msahafu ni jambo limefahamishwa na maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ

”Hakika ni juu Yetu kuikusanya na kukufanya kuweza kuisoma.”[3]

Pengine mtu akauliza ni kwa nini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuikusanya, jawabu ni kwa sababu kulikuweko na kizuizi. Kizuizi chenyewe ni kwamba Qur-aan ilikuwa ikiteremshwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maisha yake yote na wakati mwingine ilikuwa inatokea Allaah anakifuta kile anachokitaka. Wakati kulipoondoka kikwazo, Maswahabah wakaafikiana kuikusanya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu haukusanyiki juu ya upotevu.”[4]

Kuandikwa kwa elimu kumejulishwa na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ifungamanisheni elimu kwa uandishi.”[5]

Na kadhalika kuna manufaa mengine yaliyotajwa katika vitabu vya misingi.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/344).

[2]al-Muwaafaqaat (3/48) ya ash-Shaatwibiy.

[3] 75:17

[4] Kitaab-us-Sunnah (83). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (83).

[5] Swahiyh-ul-Jaamiy´ (4434).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 16/05/2023