29. Namna ya kuoanisha Hadiyth wakati wa kusujudu

Swali 29: Je, bora ni kuweka magoti kabla ya mikono wakati wa kusujudu au kinyume chake ndio bora? Ni vipi zitaoanishwa Hadiyth mbili zilizopokelewa kuhusu hilo?

Jibu: Sunnah kwa ambaye anaswali anapotaka kusujudu basi aanze magoti kabla ya mikono yake akiweza kufanya hivo kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Isitoshe hayo ndio maoni ya kikosi cha wanazuoni wengi kutokana na Hadiyth ya Waa-il bin Hujr (Radhiya Allaah ´anh) na Hadiyth nyenginezo zilizo na maana kama hiyo.

Kuhusu Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ukweli wa mambo ni kwamba haipingani na jambo hilo. Bali inaafikiana nayo. Kwa sababu ndani yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemkataza mswaliji asende chini kama anavoenda chini ngamia. Ni jambo linalotambulika kuwa anayetanguliza mikono yake amejifananisha na ngamia. Maneno yake mwishoni mwake:

“…. na aweke mikono yake kabla ya magoti yake.”

maoni yaliyo karibu zaidi na usawa ni kwamba hayo ni mageuzo yaliyowatokea baadhi ya wasimulizi. Usawa ni kwamba atangulize magoti kabla ya mikono yake. Hivo ndivo zinaoanishwa Hadiyth na sehemu ya mwisho ya Hadiyth iliyotajwa itaoanishwa na sehemu yake ya mwanzo. Mgongano unaondoka kwa njia hiyo. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amezindua juu ya maana hiyo katika kitabu chake “Zaad-ul-Ma´aad”.

Ambaye atashindwa kutanguliza magoti kutokana na maradhi au utuuzima, basi hakuna neno kwake akatanguliza mikono yake. Amesema (Subhaanah):

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninayokukatazeni basi jiepusheni nayo na nikikuamrisheni jambo basi lifanyeni muwezavyo.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

[1] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 22/08/2022