28. Swalah ya anayecheza na kutikisika kwa wingi

Swali 28: Watu wengi wanakithirisha kucheza na kutikisika ndani ya swalah. Je, kuna kiwango maalum cha kutikisika ambacho kinaharibu swalah? Je, kikomo cha kutikisika mara tatu kwa kufululiza kina msingi[1]? Kipi unachowanasihi wale wanaotikisika kwa wingi katika swalah?

Jibu: Ni lazima kwa waumini wa kiume na waumini wa kike kutulia katika swalah na kuacha kucheza. Kutulia ni katika nguzo za swalah. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ya kwamba alimwamrisha yule ambaye hakutulia katika swalah yake airudie swalah yake.”

Kilichowekwa katika Shari´ah kwa kila muumini wa kiume na muumini wa kike kuwa na unyenyekevu ndani ya swalah, kuielekea na kuhudhurisha moyo ndani yake mbele ya Allaah (Subhaanah). Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[2]

Inachukiza kucheza na nguo, ndevu au vyenginevyo. Kutokana na ninavojua kutoka katika Shari´ah takasifu jambo hilo likifanyika kwa wingi ni haramu na linaharibu swalah.

Jambo hilo halina kikomo maalum. Maoni yanayowekea mpaka hilo kwa matikisiko matatu ni dhaifu na hayana dalili. Kinachozingatiwa ni pale ambapo mswaliji mwenyewe ataona kuwa ametikisika sana. Mswaliji akiona kuwa ametikisika kwa wingi na kumefululiza, basi ni lazima kwake kuirudia swalah yake ikiwa ni swalah ya faradhi. Aidha anawajibika kutubia juu ya hilo.

Nasaha zangu kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike ni kuitilia umuhimu swalah, kunyenyekea na kuacha kucheza ndani yake ijapo ni kwa uchache tu. Hayo ni kutokana na ukubwa wa jambo la swalah, kwa sababu pia ndio nguzo ya Uislamu, ndio nguzo kuu zaidi baada ya shahaadah mbili na ndio jambo la kwanza atalofanyiwa hesabu kwalo mja siku ya Qiyaamah.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/kutikisika-mara-kwa-mara-kunabatilisha-swalah/

[2] 23:01-02

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 22/08/2022