29. Lengo la ulinganizi halihalalishi njia zake

Tumetangulia kutaja namna ambavoulinganizi umewekwa katika Shari´ah na kwamba ni ´ibaadah kubwa na tukufu. Tumetaja sharti za ´ibaadah, na kwamba Bid´ah zinaweza kuingia katika mambo ya kaida yakifanywa kwa njia ya ´ibaadah. Baada ya utangulizi huu mfupi tunaingia katika kiini cha maudhui yenyewe.

Suala la njia za ulinganizi ni kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah au si kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah ni mada ambayo wamekinzana wanazuoni wa sasa. Lipo jopo la wanazuoni linaloona kuwa mlinganizi hahitajii kulingania kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah, na kwamba inafaa kwake kutumia ule mfumo ambao anaona kuwa unatengeneza na kuwaongoza wale anaowalingania. Kwa msemo mwingine haijalishi kitu ikiwa njia yake ya kulingania inatofautiana na namna alivyolingania Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake watukufu. Maoni haya yanafasiriwa kwa njia mbili, na kila njia ina watetezi wake.

1 – Tafsiri ya kwanza ni kwamba kila mfumo na njia inayofikisha katika lengo, ambayo ni kuwarekebisha watu, inafaa kwa mlinganizi kuitumia hata kama dini imeikataza muda wa kuwa ni mwenye kufikia manufaa.

Maoni haya ni batili kutokana na tafsiri hii kwa sababu iko tayari kwenda kinyume na dini kwa ajili ya kufikia manufaa. Kufungua mlango huu kunapelekea kubadilisha mipaka na maandiko[1] yote ya dini na yanatokana na kanuni ya kiyahudi inayosema kuwa lengo linahalalisha njia. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ آمِنُوا بِالَّذِي أُنزِلَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَجْهَ النَّهَارِ وَاكْفُرُوا آخِرَهُ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

“Na kundi miongoni mwa Ahl-ul-Kitaab likasema: “Aminini yale ambayo yameteremshwa kwa wale walioamini [yaaminini] mwanzo wa mchana na yakanusheni mwisho wake, wapate kurejea.”[2]

Mfano wa tafsiri hii ni kujuzisha watu kuingia katika mabunge ya kikafiri kwa ajili ya kulingania kwa Allaah na kuwatengeneza watu na hali za jamii. Ni jambo linalotambulika kwamba kuingia katika mabunga ya kikafiri kunavunja malengo ya misingi ya dini, sembuse mambo mengine yote ya dini. Kunaibomoa dini kuanzia misingi yake na kupaka mafuta lengo lake kuu ambalo ni kumwabudu Allaah pekee.

Mfano mwingine ni kujuzisha kucheza, kuimba, kuwadhuru waislamu, kuwasemea uongo, kunyoa ndevu na kuvaa nguo yenye kuvuka kongo mbili za miguu kwa ajili ya kulingania kwa Allaah (Ta´ala)!?!?

[1] al-Mustaswfaa (1/139) ya al-Ghazaaliy.

[2] 3:72

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 35-35
  • Imechapishwa: 15/05/2023