27. Mtazamo wa ghafla wa Maswahabah wa kiume kunathibitisha nyuso za Maswahabah wa kike zilikuwa wazi

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ee ´Aliy! Usifuatishe kutazama kutazama kwingine. Una haki ya ule mtazamo wa kwanza na huna haki ya ule mtazamo wa pili.”[1]

Jariyr bin ´Abdillaah amesema:

”Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kutazama kwa ghafla ambapo akaniamrisha kugeuza macho yangu.”[2]

al-Qurtwubiy na wengine wamesema wakati walipokuwa wakitaja sababu ya kuteremshwa Aayah hii:

وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ

“Waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao.”

”Wanawake katika kipindi hicho walikuwa wanapofunika vichwa vyao basi mikia inashuka migongoni mwao, kama wanabataea, na hivyo shingo na vifua vyao vinabaki wazi. Ndipo Allaah (Subhaanah) akaamrisha kuteremsha mitandio juu ya vifua.”[3]

[1] Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, at-Twahaawiy katika ”Sharh-ul-Aathaar” na ”al-Mushkil”, al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye, al-Bayhaqiy na Ahmad kupitia kwa Shariyk, kutoka kwa Abu Rabiy´ah, kutoka kwa Ibn Buraydah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth ni nzuri na geni. Hatuitambui isipokuwa kutoka kwa Shariyk.”

Bi maana Shariyk bin ´Abdillaah al-Qaadhwiy. Ni kweli kwamba kumbukumbu yake ilikuwa mbovu, lakini hata hivyo Hadiyth imepokelewa kupitia njia nyingine. at-Twahaawiy, al-Haakim na Ahmad wameipokea kupitia kwa Hammaad bin Salamah: Muhammad bin Ishaaq ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Ibraahiym at-Taymiy, kutoka kwa Salamah bin Abiyt-Twufayl, kutoka kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia hivo. al-Haakim amesahihisha cheni yake ya wapokezi na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Kwenye cheni ya wapokezi yuko pia Ibn Ishaaq ambaye alikuwa mudallis na hakuwa akieleza anasimulia kutoka kwa nani. Hata hivyo Hadiyth ni nzuri kwa njia hizi mbili, isitoshe inatiliwa nguvu na Hadiyth ilio baada yake.

[2] Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, ad-Daarimiy, at-Twahaawiy katika ”Sharh-ul-Aathaar” na ”al-Mushkil”, al-Bayhaqiy, al-Haakim na Ahmad.

[3] al-Jaamiy´ li Ahkaam-il-Qur-aan (12/230).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 77-78
  • Imechapishwa: 13/09/2023