26. Jilbaab ilikuwa imefaradhishwa wakati wa hajj yake Mtume

Hata kama tutakadiria kuwa nimeshindwa kutilia nguvu maneno yangu, kumkubalia kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwanamke aliyeonyesha uso wake mbele ya wanamme wengine ni dalili ya wazi juu ya kufaa kwa kitendo hicho. Mambo yakishakuwa hivo basi inatambulika kuwa kimsingi ni kubaki kila hukumu kama ilivyo mpaka kuthibitishwe dalili inayoonyesha kinyume chake. Naweza kusema kuwa hakujakuja dalili kama hiyo. Bali inabaki ile hukumu ya kimsingi, kama itakavyokuja huko mbele. Yule anayedai kitu kingine ndiye ambaye anatakiwa kuleta dalili yenye kufuta. Zingatia pia kwamba tumekwishathibitisha kwa mwanamke anayetokea Khath´am; alizungumza na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj yake. Hapo ilikuwa baada ya kufaradhishwa jilbaab, jambo ambalo halina shaka. Kitu ambacho kinatilia nguvu hilo zaidi ni maneno Yake Allaah:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ

”Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao – hivyo ni utakaso zaidi kwao.”[1]

Inampa hisia msomaji ya kwamba kuna kitu kilicho wazi na ambacho kinaweza kuonekana kwa mwanamke, kwa ajili hiyo ndio maana kukaamrishwa kuteremsha macho. Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Tahadharini kukaa barabarani.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah, hatuna budi kukaa kwa sababu ya kuzungumza.”Akasema: ”Mkikataa isipokuwa kukaa basi ipeni njia haki yake.” Wakasema: ”Ni ipi haki yake, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kuinamisha macho, kuondosha maudhi, kuitikia salamu, kuamrisha mema na kukataza maovu.”[2]

[1] 24:30

[2] al-Bukhaariy (11/9), Muslim (7/3), Abu Daawuud (2/291), al-Bayhaqiy (7/89) na Ahmad (3/36) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy na Muslim na Ahmad (4/30) kupitia kwa Abu Twalhah al-Answaariy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 13/09/2023