16. Kusihi kwa swawm ya ambaye amepambaukiwa akiwa amefunga

16 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamka asubuhi hali ya kuwa na janaba inayotokana na jimaa kisha akioga na kufunga.”

Kuna maafikiano juu yake.

Imekuja katika Hadiyth ya Umm Salamah:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamka asubuhi hali ya kuwa na janaba inayotokana na jimaa kisha akioga na kufunga na wala halipi.”[1]

Hadiyth hii ni dalili juu ya kwamba mfungaji akiamka hali ya kuwa ni mwenye janaba kwa njia ya kwamba amempambazukiwa na alfajiri akiwa na janaba ya jimaa au kwa ajili ya kuota, basi swawm yake ni sahihi. Haijalishi kitu hata kama hakuoga isipokuwa baada ya kuchomoza alfajiri muda wa kuwa atajizuilia kutokamana na chakula, kinywaji na vifunguzi vyengine kwa manuizi wakati wa kuanza kufunga.

Janaba ni kila kinacholazimisha mtu kuoga kutokana na kushusha au jimaa. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[2]

Kama Allaah ametoa ruhusa ya kufanya jimaa mpaka kubainike kwa alfajiri basi hilo linapelekea uogaji uwe baada ya kupambazuka afajiri. Kufungamanishwa janaba katika Hadiyth ya kwamba inatokana na janaba ni kwa ajili ya kubainisha kwamba kuchelewesha kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) josho la janaba ni kwa kutaka kwake na kwamba hakushangazwa kwa yale yanayopelekea katika uogaji. Kwa hiyo tunapata faida kwamba si lazima kuharakisha kuoga kutokamana na janaba. Bali inafaa kuchelewesha mpaka kuingia kwa alfajiri.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuuliza na yeye huku anasikiliza kwa nyuma ya mlango ambapo akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Swalah inanikuta nikiwa na janaba. Je, nifunge?” Mtume wa Allaah akasema: “Na mimi swawm hunikuta nikiwa na janaba na nikafunga.” Akasema: “Mimi si kama wewe, ee Mtume wa Allaah! Hakika wewe Allaah amekwishakusamehe madhambi yako yaliyotangulia na yatayokuja huko mbele.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Naapa kwa Allaah kwamba hakika mimi nataraji ndiye ninayemcha Allaah zaidi katika nyinyi na mjuzi zaidi wa yale yanayopaswa kuogopwa.”[3]

Vivyo hivyo mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi ikikatika damu yake na akaona kuwa amesafika kabla ya alfajiri, basi atafunga pamoja na watu wengine ingawa hatowahi kuoga isipokuwa baada ya kuingia alfajiri. Kwa sababu wakati huo ataingia katika wale wanaotakiwa kufunga. Aidha alazimika kuharakisha kuoga ili aweze kuswali Fajr ndani ya wakati wake.

Mfungaji akiota mchana wakati amefunga basi atatakiwa kuoga na swawm yake ni sahihi. Hana khiyari wala matakwa katika jambo hilo. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah haikalifishi nafsi yoyote isipokuwa vile iwezavyo.”[4]

Ndani ya Hadiyth kuna dalili juu ya kufaa kwa mfungaji kuoga. Hapana tofauti katika hilo kati ya uogaji ambao ni wa lazima, uliyopendekezwa na ulioruhusiwa. al-Bukhaariy amesema:

“Mlango unaozungumzia kuoga kwa mfungaji.”

Kisha akataja kuwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) nguo yake ililowa maji ambapo akaivaa ilihali amefunga na ash-Sha´biy aliingia katika bafu za nje zenye maji ya moto ilihali amefunga.” al-Hasan amesema: “Hapana vibaya kwa mfungaji kusukutua kinywaji na kujitia maji apate baridi kidogo.”

Kisha akataja kuhusu maudhui haya Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotajwa mara ya kwanza[5].

Ibn-ul-Munayyir al-Kabiyr ametaja chini ya mlango uliotajwa:

“Ndani yake kuna Radd kwa yule ambaye anaona kuwa imechukizwa kwa mfungaji kuoga. Akichukizwa na hilo kwa kuchelea maji yasifike kooni sababu hiyo inabatilishwa kwa kusukutua, kuswaki na kwa kuonja chakula na mfano wa mambo hayo. Akichukizwa na hilo kwa sababu ya anasa basi atambue kuwa Salaf wamependekeza kwa mfungaji anasa na kujipamba kwa kutengeneza nywele zake, kujipaka mafuta, wakajuzisha kujipaka wanja na mengineyo. Ndio maana ametaja matendo haya[6] chini ya kichwa cha khabari cha uogaji.”[7]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ee Allaah! Tupitishe njia ya wale wenye kukutii, tuwafikishe kuthibiti na kunyooka juu yake, tuepushe na yale yanayopelekea katika hasara na majuto, tusalimishe na khofu siku ya Qiyaamah, tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1925) na Muslim (1109).

[2] 02:187

[3] Muslim (1110).

[4] 02:286

[5] Fath-ul-Baariy (04/153).

[6] Matendo anayokusudia ni Siwaak, kuonja chakula, kujipaka mafuta na mengineyo. Ametaja mapokezi kutoka kwa Salaf juu ya kufaa kuyafanya.

[7] al-Mutawaariy ´alaa Taraajim-il-Bukhaariy, uk. 131 ya al-Munayyir.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 28/04/2022