15 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alijiliwa na bwana mmoja akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Kipi kimekuangamiza? Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ndani ya Ramadhaan.” Akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Kaa chini” na bwana yule akakaa chini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaletewa chombo kilicho na tende ambapo akasema: “Zitoe swadaqah.” Bwana yule akasema: “Hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko sisi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Zichukue na ukawalishe familia yako.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth hii ni dalili juu ya ukubwa wa dhambi ya mfungaji kufanya jimaa mchana wa Ramadhaan kwa sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuyakubali maneno ya bwana yule aliposema:

“Nimeangamia.”

Bi maana nimetumbukia ndani ya dhambi kwa kufanya yale niliyoharamishiwa kuyafanya ndani ya swawm. Imekuja katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba alisema:

“Nimeungua.”[2]

Pia imefahamisha kuwa ambaye atamjamii mke wake mchana wa Ramadhaan ilihali amefunga ya kwamba inaharibika funga yake akiwa amekusudia na mwenye kukumbuka kuwa amefunga. Vilevile analazimika kulipa siku hiyo ambayo ameiharibu kwa jimaa pamoja na kutubu tawbah ya kweli. Aidha analazimika kutoa kafara kali kutokana na dhambi aliyokiri mwenyewe; nayo inakuwa kwa mpangilio: kuacha mtumwa huru muumini, asipopata basi anatakiwa kufunga miezi miwili kwa kufuata, asipoweza basi anatakiwa kuwalisha masikini sitini ambapo kila masikini atampa Mudd[3] ya ngano nzuri. Kiwango cha Mudd ni gramu 563. Inasihi pia kutoa mchele na chakula chengine ambacho kinaliwa kwa wingi katika mji.

Akijamiiana kwa kusahau basi swawm yake ni sahihi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hatolazimika kulipa wala kutoa kafara. al-Bukhaariy amesema:

“al-Hasan na Mujaahid wamesema kuwa akijamiiana kwa kusahau basi hakuna kinachomlazimu.”[4]

Vivyo hivyo akijamiiana wakati wa kupambazuka kwa alfajiri hali ya kuamini kuwa bado ni usiku na baadaye ikambainikia kuwa alfajiri imekwishaingia, halazimiki kulipa wala kutoa kafara kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maoni haya ndio sahihi zaidi na yanayofanana na misingi ya ki-Shari´ah na dalili ya Qur-aan na Sunnah. Pia ndio kipimo cha misingi ya Ahmad na wengineo. Kwani hakika Allaah hamuadhibu mtu aliyesahau na aliyekosea. Huyu amekosea. Allaah amehalalisha kula na jimaa mpaka ubainike uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi. Ambaye atafanya yale yaliyosuniwa kwake na akahalalishiwa hafungui. Huyu ana haki zaidi ya kusamehewa kuliko msahaulifu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.”[5]

Hii ni hukumu ya mwanamme. Kuhusu mwanamke yeye swawm yake inaharibika na analazimika kulipa kwa hali yoyote. Ama kuhusu kafara itamlazimu ikiwa ameridhia kufanya hivo. Na akiwa ametenzwa nguvu basi hakuna kinachomlazimu.

Mume akimjamii mke katika swawm ya kulipa deni la Ramadhaan basi swawm yake inaharibika. Katika hali hiyo atalazimika kulipa pamoja na kutubu lakini hahitajii kutoa kafara. Kwa kuwa kafara ni kitu maalum kipindi cha jimaa mchana wa Ramadhaan. Ni kitu kina heshima na utukufu wake maalum. Kufungua ni kukiuka ile heshima na utukufu. Hilo ni tofauti na ulipaji ambao masiku ni yenye kulingana kwa nisba yake[6]. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ee Allaah! Tukinge kutokamana na sababu za kwenda kinyume na kuasi, turuzuku kuhakiki imani kwa njia itayokufanya uturidhie, utusamehe tuliyotanguliza na tuliyochelewesha, tuliyoyafanya kwa siri na tuliyoyafanya kwa wazi na yale ambayo Wewe unayajua zaidi kuliko sisi, utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

[2] Muslim (1112).

[3] Hayo yamepokelewa katika baadhi ya mapokezi katika kisa cha mjamiaji:

”Akaletewa chombo kilichokuwa na pishi kumi na tano.” Rejea ”Fath-ul-Baariy” (04/69).

[4] Fath-ul-Baariy (04/155-156). Tazama ”Taghliyq-ut-Ta´liyq” (03/156-157) na ”ad-Durar as-Saniyyah” (02/22).

[5] Majmuu´-ul-Fataawaa (25/264).

[6] al-Kaafiy (01/357) na ”ad-Durar as-Saniyyah” (03/388).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 28/04/2022