14 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ambaye yatamshinda matapishi basi halazimiki kulipa. Na ambaye atajitapisha basi ni lazima kwake kulipa.”[1]

Wapokezi wake ni waaminifu.

Hadiyth hii ni dalili juu ya kwamba mfungaji akijitapisha swawm yake inaharibika na analazimika kulipa. Haya ndio maoni ya kikosi cha wanazuoni wengi. Lakini yakimshinda na yakamtoka bila kutaka kwake swawm yake ni sahihi. al-Khattwaabiy amesema:

“Sijui tofauti kwa wanazuoni juu ya jambo hilo.”[2]

Ibn Qudaamah amesema:

“Haya ndio maoni ya wanazuoni wote.”[3]

Maana ya:

“… atajitapisha.”

Bi maana amesababisha kutoka kwake kwa makusudi. Maana ya:

”Ambaye yatamshinda… ”

Bi maana yamemshinda na yamemtangulia kutoka.

Akitapika kwa makusudi anafungua. Ni mamoja matapishi yatakuwa mengi au madogo kutokana na udhahiri wa Hadiyth. Jengine ni kwa sababu vifunguzi vengine hakuna tofauti kati ya vingi vyake na vichache vyake. Muwaffaq Ibn Qudaamah amesema:

“Hakuna tofauti kati matapishi yawe aina ya chakula, machungu, makohozi, damu au kitu kingine. Yote yanaingia chini ya uneaji wa Hadiyth. Allaah ndiye mjuzi zaidi wa usawa.”[4]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema alipokuwa akibainisha hekima ya kufungua kwa kutapika:

“Mfungaji amekatazwa kuchukua chakula na kinywaji kinachomfanya kupata nguvu. Amekatazwa kukitoa nje kile kinachomdhoofisha na kukitoa chakula chake ambacho kwacho anakula. Vinginevyo akiwezesha jambo hilo basi linakuwa lenye kumdhuru na anakuwa mwenye kuchupa mpaka katika ´ibaadah yake na hakufanya uadilifu.”[5]

Baadhi ya wanazuoni wameona kuwa matapishi hayafunguzi. Haya ni maoni ya Ibn ´Abbaas na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhum). Aidha ´Ikrimah. Pia ni upokezi kutoka kwa Imaam Maalik. Pia ndio udhahiri wa uchaguzi wa al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah)[6]. Kwa sababu haikusihi chochote juu ya hayo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) licha ya kwamba matapishi ni kitu kinachotokea mara nyingi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Akitapika basi asifungue. Hakika si venginevyo inatoka na wala haipenyi.”[7]

Ee Allaah! Tuwafikishe kwenye njia ya utiifu, ututhibitishe juu ya kufuata Sunnah na kulazimiana na mkusanyiko na wala usitufanye kuwa miongoni mwa wenye kuitambua haki na wakaipoteza, utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] Abu Daawuud (2380), at-Tirmidhiy (720), Ibn Maajah (01/536), Ahmad (16/283), al-Haakim (01/427) na wengineo kupitia kwa ´Iysaa bin Yuunus. Hishaam bin Hassaan ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Siyriyn, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye ameisimulia. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. ad-Daaraqutwniy amesema (02/84):

”Wapokezi wake wote ni waaminifu.”

Lakini ni Hadiyth ambayo iko na kasoro iliyojificha. Wamesema hivo Ahmad, al-Bukhaariy, ad-Daarimiy, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na wengineo na wakasema:

“Haikuhifadhiwa. Kwa sababu Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amefutu kinyume na hivo, kama itavokuja huko mbele. Kama inavotambulika jumla ya wapokezi wake ni waaminifu. Haimaanishi kuwa Hadiyth ni Swahiyh.

[2] Ma´aalim-us-Sunan (03/261).

[3] al-Mughniy (04/368).

[4] al-Mughniy (04/369).

[5] Majmuu´-ul-Fataawaa (25/250).

[6] Fath-ul-Baariy (04/173).

[7] al-Bukhaariy hali ya kuiwekea taaliki (04/173 – Fath-ul-Baariy) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 28/04/2022