13 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau si [kuchelea] kuwatia uzito Ummah wangu basi ningewaamrisha kutumia Siwaak wakati wa kila swalah.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

al-Bukhaariy ameipokea kwa cheni ya wapokezi pungufu:

“Lau si [kuchelea] kuwatia uzito Ummah wangu basi ningewaamrisha kutumia Siwaak wakati wa kila kutawadha.”

Hadiyth hii ni dalili juu ya makokotezo ya Siwaak wakati wa kila swalah. Ni mamoja swalah hiyo ni ya faradhi au ni swalah iliyopendekezwa. Hapana tofauti katika hilo kati ya mfungaji na mwengine, mwanzoni mwa mchana na mwishoni mwake. Lengo ni ili mfungaji aingie ndani ya ´ibaadah akiwa katika sura nzuri na ananukia vizuri.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

Siwaak inasafisha mdomo na ni yenye kumridhisha Mola.”[2]

Hili ni lenye kuenea na linamuhusu aliyefunga na ambaye hakufunga. Ni lazima kuitendea kazi kutokana na kuenea kwake mpaka kuthibiti umaalum wake. Kuenea kwake hakuna umaalum sahihi. Ibn-ul-´Arabiy amesema: “Wanazuoni wetu wamesema:

“Kuhusu mfungaji kutumia Siwaak hakukusihi Hadiyth Swahiyh hali ya kukanusha wala kuthibitisha. Isipokuwa tu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesisitiza Siwaak zaidi wakati wa kila mtu anapotawadha na kila mtu anaposwali kwa njia ya kuachia pasi na kutafautisha kati ya mfungaji na asiyekuwa mfungaji. Amekokoteza kutumia Siwaak siku ya ijumaa na hakutofautisha kati ya mfungaji na mwengine. Huko mbele tumetanguliza faida zake kumi katika usafi ijapo mfungaji ana haki zaidi ya kuitumia.”[3]

Maoni yanayosema kuwa imesuniwa kwa mfungaji kutumia Siwaak ndio yenye nguvu zaidi katika suala hili. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Machukizo ya kutumia Siwaak baada ya kupondoka jua hayajasimama juu ya dalili inayokubalika ki-Shari´ah inayosilihi kuyafanya maalum yale maandiko yaliyotaja Siwaak kwa njia yenye kuenea.”[4]

Wale waliosema kuwa imechukizwa kwa mfungaji kutumia Siwaak baada ya jua kupinduka wamejengea hoja kwa Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mkifunga basi swakini asubuhi na wala msiswaki jioni.”[5]

 Jioni (العَشِيُّ) ni mwishoni mwa mchana baada ya jua kupondoka mpaka wakati wa magharibi. Hadiyth hii ni dhaifu.

Vilevile wamejengea hoja kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah iliokwishatangulia. Ndani yake kumetajwa:

“Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”[6]

Namna ya kujengea hoja wamesema (الخُلوف) ni ile harufu mbaya inayokuwa mdomoni wakati tumbo linakuwa halina chakula. Hili mara nyingi hudhihiri mwishoni mwa mchana. Ikiwa ni yenye kupendwa na Allaah (Ta´ala) inakuwa ni yenye kusifiwa ki-Shari´ah. Imetokana na kumtii Kwake. Kwa hivyo haitakikani aendelee kutumia Siwaak. Hii sio dalili. Kwa sababu harufu mbaya inatokana na tumbo kuwa tupu na baada ya kukiacha chakula, kitu ambacho hakiondoki kwa kutumia Siwaak. Isitoshe ni yenye kupendwa na Allaah kwa ajili ya kutanguliza mbele radhi Zake kwa kuacha matamanio kwa yale anayoyapenda mtu. Si jambo lenye kupendeza kwa Allaah kwa kule kuacha uchafu mdomoni na kwenye meno. Jengine ni kwamba wako wafungaji ambao kimsingi haiwaondoki ile harufu mbaya. Hilo ima ni kwa sababu ya tumbo lake kuwa tupu au kwa sababu tumbo lake halisagi chakula kwa haraka. Kwa hivyo ile harufu mbaya inaweze kupatikana kabla ya jua kupinduka.

Ni uzuri ulioje wa yale yaliyopokelewa kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Ghanm ambaye amesema: “Nilimuuliza Mu´aadh bin Jabal: “Je, niswaki nikiwa nimefunga?” Akasema: “Ndio.” Nikasema: “Mchana?” Akajibu: “Asubuhi au jioni.” Nikasema: “Watu wanachukizwa na jambo hili jioni na wanasema kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”

Akasema: “Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu! Amewaamrisha waswaki na hakuwaamrisha wakusudie kuacha vinywa vyao vinukie vibaya… hakuna chochote chenye kheri katika jambo hilo. Bali ndani yake mna shari.”[7]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ee Allaah! Fanya uzuri wa matendo yetu yawe ni yale ya mwisho yake, uzuri wa matendo yetu yawe ni yale mwisho wake, uzuri wa masiku yetu ni ile siku tutakutana Nawe, tufishe ilihali uko radhi Nasi, utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (847) na Muslim (252).

[2] an-Nasaa´iy (01/10) na Ahmad (40/240). al-Bukhaariy ameipokea kwa cheni ya wapokezi pungufu hali ya kukata (04/15) katika “al-Fath”. Zipo Hadiyth nyingi zinazoitia nguvu Hadiyth hii kutoka kwa jopo la Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Tazama “Jaamiy´-ut-Tirmidhiy” (01/35) na “Takhiysw-ul-Khabiyr” (01/70).

[3] ´Aaridhwat-ul-Ahwadhiy (03/256) na katika (01/40) ametaja faida za Siwaak.

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (25/266).

[5] ad-Daaraqutwniy (02/204), al-Bayhaqiy (04/274) kupitia kwa Kaysaan, kutoka kwa Yaziyd bin Bilaal, kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Swahabah. Pia kutoka njia ya Kaysaan, kutoka kwa ´Amr bin ´Abdir-Rahmaan, kutoka kwa Khabaab kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (04/78). Ameipokea pia ad-Dulabiy katika “al-Kunaa” (02/52) kutoka kwa ´Aliy kutoka kwa Swahabah. ad-Daaraqutwniy amesema:

“Kaysaan Abu ´Umar hana nguvu. Hatambuliki yule aliyeko kati yake yeye na ´Aliy.”

al-Bayhaqiy amesema maneno kama hayo. Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw” (01/73):

“Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu.”

[6] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151) na (164) na tamko ni lake.

[7] at-Twbaraaniy katika ”al-Kabiyr” (20/70-71). Katika cheni ya wapokezi wake yuko Bakr bin Khunays al-Kuufiy mfanya ´ibaadah. Wengi wanamdhoofisha. Ibn Ma´iyn amemfanya kuwa mwaminifu. Tazama ”Tahdhiyb-ul-Kamaal” (04/208).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 38-40
  • Imechapishwa: 28/04/2022