Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

”Kwa mujibu wa Hadiyth hii dogo liwezalo kusemwa ni kwamba ni haramu kujifananisha nao, ijapo udhahiri wake unapelekea kwamba yule mwenye kujifananisha nao amekufuru. Kama alivosema Allaah:

وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ

”Na yeyote atakayewafanya marafiki basi yeye ni katika wao.”[1]

Haya yanafanana na maneno yake ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh):

”Yule anayejenga katika mji wa washirikina, akasherehekea Nayruuz na Mahrajaan na akajifananisha nao mpaka akafa, atafufuliwa na kukusanywa nao siku ya Qiyaamah.”

Maneno haya yanaweza kufasiriwa kwa kule kujifananisha moja kwa moja, jambo ambalo linapelekea katika ukafiri na kuharamisha sehemu ya kujifananisha. Yanaweza vilevile kufahamika kuwa ni miongoni mwao katika kile kiwango tu ambacho amejifananisha nao. Ikiwa kujifananisha ni ukafiri, dhambi au alama, basi hukumu yake itafuatia hilo. Kwa hali yoyote ni haramu kujifananisha nao kwa ajili tu ya kujifananisha nao.

Kujifananisha kunaweza kukusudia yule anayefanya kitu kwa sababu tu wamekifanya kitu hicho, kama inavyodhihiri, na ambaye anawafuata wengine kutokana na lengo fulani, kwa sharti jambo hilo liwe limechukuliwa kutoka kwa wengine. Hata hivyo ni jambo linahitaji kuangaliwa vyema kuhusu mtu ambaye amefanya jambo na wakawepo wengine pia waliolifanya pasi na kuwepo yeyote katika wao ambaye amelichukua kutoka kwa mwengine. Hata hivyo jambo hilo linaweza kukatazwa, mosi kwa ajili ya kuchukua tahadhari na pili kwa ajili ya kujitofautisha. Mfano wa hilo ni kama kuzipaka rangi ndevu na kukata masharubu. Ingawa maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Zibadilisheni na wala msijifananishe na mayahudi.”

kunafahamisha kuwa mtu anaweza kujifananisha nao endapo ataacha kubadilisha kitu kilichoanzishwa na sisi. Hili lina mkazo zaidi kuliko kufanya jambo ambalo linafanywa na wao. al-Qaadhwiy Abu Ya´laa amepokea kuwa Ibn ´Umar amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kujifananisha na wasiokuwa waarabu na akasema:

”yeyote mwenye kujifananisha na watu, basi yeye ni katika wao.”

Wanazuoni wengi wameitumia Hadiyth hii kuchukizwa na mambo ambayo ni katika ya wasiokuwa waislamu.”

Kisha akataja baadhi ya nukuu kutoka kwa Ahmad na wengineo:

”Muhammad bin Abiy Harb amesema: ”Ahmad aliulizwa kuhusu ndala zinazotoka Sindh na kama inafaa kwa mtu kutoka nazo nje. Akachukizwa na kitendo hicho, kwa wanaume na kwa wanawake, lakini akasema: ”Isipokuwa kama zitatumiwa chooni na wakati wa kutawadha.” Bi maana katika hali hiyo hazina neno. Akasema: ” Nachukizwa na ndala zinazogongagonga. Ni mambo ya wasiokuwa waarabu.”

[1] 5:51

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 204-205
  • Imechapishwa: 28/11/2023