14. Sababu ya kumi na tatu ya maisha mazuri: Faida mbili kuu

13- Katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini wa kiume asimchukie muumini wa kike. Akichukia kutoka kwake tabia moja basi atafurahishwa na tabia nyingine.”[1]

zipo faida mbili kuu:

1- Kuna maelekezo ya namna ya kutaamiliana na mke, ndugu, rafiki na mfanya kazi na kila yule ambaye kati yako wewe na yeye kuna mafungamano na mawasiliano na kwamba unatakiwa kuiandaa nafsi juu ya kwamba ni lazima atakuwa na kasoro, upungufu au kitu unachokichukia. Ukiona jambo hilo basi linganisha kati ya jambo hilo na yale yanayokulazimu au yanayokupasa katika mafungamano yenye nguvu au kubaki kupendana kwa kukumbuka yale mazuri yake na makusudio maalum na yaliyoenea. Kwa njia hii ya kufumbia macho yale mabaya na kuyatazama yale mazuri urafiki na mawasiliano yanadumu na raha itatimia na utaipata.

2- Kuondosha misononeko, masikitiko na kubakia usafi na kudumu katika kuzisimamia zile haki ambazo ni za lazima na zilizopendekezwa. Pia kunapatikana raha kati ya pande mbili. Yule asiyetaka mwongozo kwa haya aliyotaja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bali akayapindua mambo na kazi yake ikawa ni kuyazingatia yale mapungufu na akayamfumbia macho yale mazuri, basi ni lazima aingie mashakani. Ni lazima yachafuke yale mafungamano na mapenzi yaliyoko baina yao na zikatike nyingi katika zile haki ambazo inatakiwa kila mmoja katika wao azihifadhi.

Watu wengi wenye hima kubwa huziandaa nafsi zao wakati wa kutokeza yale mambo ambayo ni mazito na yale mambo yanayotikisa juu ya kuwa na subira na utulivu. Lakini utaona wanakuwa ni wenye kubabaika katika yale mambo ambayo ni madogo na mepesi. Matokeo yake nafsi yake iliyosafi ikachafuka. Sababu ya jambo hili ni kwamba wao wameziandaa nafsi zao juu ya yale mambo ambayo ni makubwa na wakaziacha juu ya yale mambo ambayo ni madogo. Hivyo yakawadhuru na kuwaathiri katika raha zao.

Mwerevu na mshupavu ni yule mwenye kuiandaa nafsi yake juu ya yale mambo ambayo ni madogo na makubwa na wakati huohuo anamuomba Allaah msaada juu yake na kwamba asimwache akaitegemea nafsi yake muda wa kupepesa kwa jicho. Hapo ndipo litawapesika kwake jambo dogo na kubwa na aidha atakuwa ni mwenye nafsi iliyotulizana na mwenye moyo wenye kutulia na wenye furaha.

[1] Muslim.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 24/06/2020