13. Sababu ya kumi na mbili ya maisha mazuri: Kumtegemea Allaah

12- Pale ambapo moyo utaegemea kwa Allaah, ukamtegemea na usijisalimishe na mawazo wala usimilikiwe na ujengeka wa fikira ambazo ni mbaya na sambamba na hilo ukamwamini Allaah na ukajenga matumaini katika fadhilah zake, basi ataondokewa na misononeko na masikitiko yote. Aidha ataondokewa na mengi katika maradhi ya kiwiliwili na ya kimoyo na pia moyo utapata kuwa na nguvu na kukunjuka kiasi kisichoweza kuelezwa.

Ni hospitali ngapi zimejaa wagonjwa wa mawazo na wenye kujenga fikira mbaya! Ni kwa kiasi gani mambo haya yameziathiri nyoyo za wengi wenye nguvu sembuse wanyonge! Ni kwa kiasi gani yamepelekea katika upumbavu na wendawazimu! Msalimishwaji ni yule aliyesalimishwa na Allaah na akawafikishwa kupambana na nafsi yake ili kuweza kufikia sababu zenye manufaa zenye kuutia nguvu moyo wake na zenye kuondosha ule wasiwasi wake. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Yeyote anayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[1]

Bi maana atamtosheleza kutokana na yote yenye kumsumbua katika mambo ya dini na dunia yake.

Yule mwenye kumtegemea Allaah anakuwa na moyo wenye nguvu. Haathiriwi na fikira na wala hayumbishwi na matukio kwa sababu ya kutambua kuwa hayo yanatokana na unyonge wa nafsi na kutokamana na woga na khofu usiyokuwa na ukweli wowote. Pamoja na hayo anatambua kuwa Allaah amebeba jukumu la kumtosheleza kikamilifu kwa yule mwenye kumtegemea yeye. Hivyo anamtegemea Allaah na anakuwa na utulivu wa ahadi Yake. Kwa ajili hiyo huzuni na wasiwasi wake unaondoka na magumu yake yanageuka kuwa mepesi, huzuni yake inageuka kuwa furaha, khofu yake inageuka kuwa amani.

Tunamuomba Allaah afya na atutunuku moyo wenye nguvu, uimara kwa kumtegemea kikamilifu ambako Allaah amechukua dhamana kwa watu wake kwa kila kheri na kuondosha kila lenye kuchukiza na lenye madhara.

[1] 65:03

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 24/06/2020