Hammaad bin Salamah ameeleza kutoka kwa Abiy Sinaan ´Iysaa bin Sulaymaan al-Qasmaliy amesema:
“Nilimzika mwanangu Siynaan, Abu Twalhah al-Khawlaaniy alikuwa amekaa pembizoni mwa kaburi. Wakati nilipotaka kutoka, alinishika mkono na kusema: “Nisikupe bishara njema?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “”adh-Dhwahhaak bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Azrab amenihadithia, kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Anapofariki mtoto wa mja Wangu, basi Allaah huwaambia Malaika Wake: “Mmemfisha mtoto wa mja Wangu.” Wakajibu: “Ndio.” Akasema: “Mmechukua rundo la moyo wake?” Wakajibu: “Ndio.” Akasema: “Amesema nini mja Wangu?” Wakajibu: “Amekuhimidi na akasema: “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”.” Allaah husema: “Mjengeeni mja wangu nyumba Peponi na iiteni jina “Nyumba ya himdi”.”[1]
Ameipokea at-Tirmidhiy.
Zayd bin Aslam amesema:
“Mtoto wa Daawuud (´alayhis-Salaam) alifariki ambapo akahuzunika huzuni kubwa. Allaah (Taa´ala) akamteremshia Wahy: “Mtoto huyu alikuwa analingana na nini kwako?” Akajibu: “Ee Mola! Mtoto huyu kwangu alikuwa analingana na dhahabu iliyojaa ardhi.” Ndipo Akamwambia: “Basi badala yake siku ya Qiyaamah unapata Kwangu thawabu zilizojaa ardhi.”
Baadhi ya yale tuliyoyataja na kuyapokea katika yale yaliyo na maana yake yanamliwaza yule aliyefikwa na msiba ambaye Allaah amemwongoza. Imepokelewa namna ambavyo wapo wanazuoni wengi na wafanya ´ibaadah ambao walitamani watoto wao wafe kutokana na wanavyojua yale malipo alionayo yule mwenye kufikwa na msiba kwa jambo hilo.
Abul-Ahwas ´Awf bin Maalik al-Jushamiy amesema:
“Tuliingia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye alikuwa na wavulana wake watatu, wazuri kama dirhamu nzuri. Tukawa tunashangazwa na uzuri wao ambapo akatwambia: “Inaonekana ni kama vile mnanionea wivu.” Wakasema: “Ndio, tunaapa kwa Allaah. Muislamu anaona wivu kwa watu kama hawa.” Akainua kichwa chake juu ya nyumba yake ndogo, akatazama juu kwenye kiota cha ndege ambapo mbayuwavu alitaga mayai na akasema: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Kupangusa vumbi mikono yangu kutokana na vumbi la makaburi yao kunapendeza zaidi kwangu kuliko kuacha kiota cha mbayuwayu kianguke chini ardhini, na yakavunjika mayai yake.”[2]
Abu Muslim al-Khawlaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:
“Kumpata mtoto ambaye Allaah atamwangalia makuzi yake mpaka pale atakapokuwa barobaro na akawa ndiye ninayempenda zaidi na baadaye Allaah akamchukua kutoka kwangu kunapendeza zaidi kwangu kuliko kuwa na dunia na vilivyomo ndani yake.”
Imepokelewa kwamba ´Abdullaah bin Shawdhab al-Balkhiy alikuwa na mtoto na alikuwa amekaribia miaka ya baleghe. Akamtuma mjumbe kwa watu wake na kusema:
“Nitaomba du´aa na muitikie “Aamiyn!” juu ya du´aa yangu. Wakasema, ndio. Akamuomba Allaah amchukue mtoto wake, na isitoshe alikuwa hana mtoto mwingine. Watu wale wakaitikia “Aamiyn!” kisha baadaye wakasema: “Ee baba fulani! Ni kipi kilichokupelekea ufanye hivo ilihali huna mtoto mwingine zaidi yake?” Akasema: “Nimeota kana kwamba watu wamekusanyika siku ya Qiyaamah na watu wakapatwa na joto kali na kiu kikali. Tahamaki nikaona watoto wanatoka Peponi, wamebeba mitungi na vikombe vina kinywaji. Nikamuona mtoto wa kaka yangu na nikasema: “Ee fulani! Mnyweshe maji ami yako!” Ndipo akasema: “Ee ami! Hakika sisi hatuwanyweshi maji isipokuwa baba na mama zetu.” Akasema: “Ndio nikapenda Allaah anipe mtangulizi.” Baada ya kipindi fulani mtoto yule akafariki.”[3]
[1] at-Tirmidhiy (1021). Nzuri kwa mujibu wa Ibn Hajar katika ”Nataa-ij-ul-Afkaar” (3/285) na al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (1021).
[2] at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (9/113). al-Haythamiy amesema:
“Wanamme wa at-Twabaraaniy ni wanamme wa Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaa-id (7/285))
[3] Shu´b-ul-Iymaan (7/139-140) ya al-Bayhaqiy.
- Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 76-80
- Imechapishwa: 16/08/2023
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)