13. Bwana mrefu kwenye bustani

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Bwana mmoja katika Answaar alikuwa na mvulana aliyekuwa akimfuata anapoenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Unampenda?” Akajibu: “Ndio, ee Mtume wa Allaah! Allaah akupende kama jinsi ninavyompenda.” Akasema: ”Hakika Allaah (Ta´ala) ananipenda zaidi kuliko wewe unavyompenda.”Hakukupita kitambo kirefu mtoto yule akaaga dunia. Akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuonyesha masikitiko yake.  Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Je, wewe huridhii mtoto wako kuwa pamoja na mtoto wangu Ibraahiym na akicheza naye chini ya ´Arshi?” Akasema: ”Ndio bila shaka, ee Mtume wa Allaah.”[1]

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr”.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watoto wa waumini wanaangaliwa na Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) Peponi.”[2]

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake.

Katika Hadiyth ndefu Samurah bin Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ndoto kutoka kwa Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Usiku wa leo nilijiliwa na wawili waliokuja na wakanituma…Tukapita katika bustani ya giza lililokuwa na kila mwanga wa masika. Ndani ya bustani alikuwepo mwanamme mrefu ambaye nakaribia kutoona kichwa chake kutokana na urefu mpaka mbinguni. Pembezoni na mtu huyo kulikuwepo mkusanyiko wa watoto ambao kamwe sijawahi kuuona… Bwana huyo mrefu kwenye bustani alikuwa ni Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Ama kuhusu watoto waliokuwa wamemzunguka ni kila mtoto aliyekufa juu ya maumbile.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy kwa kirefu, Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy.

Abu Nu´aym al-Aswbahaaniy amepokea kupitia kwa at-Twabaraaniy kwa cheni ya wapokezi laini kupitia kwa Subayh bin al-´Alaa’, kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Itapokuwa siku ya Qiyaamah kutanadiwa kati ya watoto wa waislamu: “Tokeni nje ya makaburi yenu.” Watatoka nje ya makaburi yao. Kisha kutanadiwa kati yao: “Nendeni Peponi kwa vikundi.” Watasema: “Ee Mola wetu! Pamoja na wazazi wetu?” Kisha kutanadiwa kati yao: “Nendeni Peponi kwa vikundi.” Watasema: “Ee Mola wetu! Pamoja na wazazi wetu?” Kutanadiwa kwa mara ya tatu: “Pamoja na wazazi wenu.” Kila mtoto ataenda kwa wazazi wake, watawashika mikono yao na kuwaingiza Peponi. Siku hiyo watakuwa ni wenye kuwatambua vyema zaidi wazazi wao kuliko watoto wenu waliokuwa katika majumba yenu.”

Ni uzuri uliyoje mtu alivyompa rambirambi rafiki yake juu ya mtoto wake aliyeaga dunia aliposema:

Ikiwa unalia kwa ajili ya kumnufaisha,

basi haraka amekwishaingia Pepo ya kudumu

Na ikiwa unalia kwa ajili ya kujinufaisha wewe,

basi mtoto wako ameshakuwa mwombezi

[1] at-Twabaraaniy (3/10), Ibn Hibbaan (725) na al-Haakim (1/384) ambaye amesema:

”Cheni ya wapokezi ya Hadiyth ni Swahiyh.”

[2] Ahmad (2/326), Ibn Hibbaan (1826) na al-Haakim (1/384) ambaye amesema:

”Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Tazama “as-Swahiyhah” (603).

[3] al-Bukhaariy (4047), Muslim (2275), at-Tirmidhiy (2294) na an-Nasaa’iy (4/82).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 72-76
  • Imechapishwa: 16/08/2023