12. Mwanao akikusubiri nje ya mlango wa Peponi

Mu´aawiyah bin Qurrah ameeleza kutoka kwa baba yake aliyesema:

”Bwana mmoja alikuwa akija na mtoto wake wa kiume kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Unampenda?” Akajibu: “Ee Mtume wa Allaah! Allaah akupende kama jinsi ninavyompenda.” Ghafla Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa hamuoni yule mtu. Akasema: “Vipi kuhusu mtoto wa fulani?” Wakamwambia: “Amefariki, ee Mtume wa Allaah!” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia baba yake: “Hupendi kuingia moja katika milango ya Peponi na kukuta kuwa anakusubiri?” Mtu mmoja akasema: “Yanamuhusu yeye mwenyewe, ee Mtume wa Allaah, au na sisi pia?” Akajibu: “Yanawahusu nyinyi nyote.”[1]

Ameipokea Ahmad katika “al-Musnad” yake.

Kwa an-Nasaa’iy, at-Twabaraaniy na wengineo imekuja:

“Ilikuwa pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokaa, basi wanakaa pamoja naye kundi la Maswahabah wake. Kati yao alikuwepo bwana mmoja ambaye alikuwa na mtoto wa kiume mdogo aliyekuwa akimjia kwa nyuma yake akamkalisha mbele yake.  Hatimaye mtoto yule akafariki. Bwana yule akawa anamfikiria, akimuhuzunikia mtoto wake ambapo akaacha kuwa anadhuhuria vikao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaona kuwa anakosekana akasema: ”Kwa nini simuoni fulani?” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Mtoto wake, uliyekuwa ukimuona, ameaga dunia. Hilo limemzuia kuhudhuria vikao. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakutana naye na akamuuliza juu ya kijana wake. Akamweleza kuwa ameaga dunia ambapo akampa pole. Kisha akasema: ”Ee fulani! Ni kipi kinachopendeza zaidi kwako ustareheshwe naye kipndi cha umri wako uliyobaki au kesho ufike kwenye mlango miongoni mwa milango ya Peponi umkute amekwishakutangulia huko na kukufungulia?” Akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Napendelea zaidi anitangulie katika mlango wa Peponi ambapo anifungulie.” Akasema: ”Basi hilo ni lako.” Bwana mmoja katika Answaar akasimama na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Allaah anifanye mimi ni fidia kwako. Hili linamuhusu fulani mwenyewe au waislamu wote wanaofiwa na watoto wao wadogo?” Akasema: ”Bali ni kila muislamu anayefiwa na mtoto mdogo.”[2]

Hassaan bin Kurayb amesema:

”Kuna mtoto kati yao aliyekufa, hivyo baba yake akasononeka mno. Hawshab, ambaye ni Swahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akasema: ”Nisikueleze niliyomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema kuhusu mfano wa hali ya mwanao? Kuna mmoja katika Maswahabah alikuwa na mtoto wa kiume ambaye ameshainukia na alikuwa akija na baba yake kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadaye akafariki. Baba yake akahuzunika kwelikweli karibu siku sita. Haji kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye akasema: ”Mbona simuoni fulani.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Mtoto wake amekufa na hivyo akamsononekea.” Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona, akasema: ”Inakupendeza mwanao hivi sasa awe mwenye uchangamfu, mwerevu, shujaa na kijana bora kabisa, au uambiwe: ”Ingia Peponi kutokana na malipo Tuliyochukua kutoka kwako?”[3]

Ameipokea Abu Nu´aym katika “al-Ma´rifah” na ipo katika “al-Mu´jam” ya Ibn Qaaniy´ na wengineo.

´Abdullaah bin Buraydah ameeleza kuwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipokuwa na taarifa ya kufariki mtoto wa mwanamke mmoja katika Answaar. Akasimama na sisi pia tukasimama. Alipomuona mwanamke yule akasema: ”Ni mahuzuniko gani haya?” Akasema: ”Ni vipi nisiwe na mahuzuniko, ee Mtume wa Allaah, ilihali hawaishi watoto wangu?” Akasema: ”Ni watoto wa mwanamke kama huyo ndiye wanaoeshi. Je, hivi hupendi kumuona kwenye mlango wa Peponi huku akikwita?” Mwanamke yule akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Itakuwa hivo.”[4]

[1] Ahmad (3/436) na (5/34-35).

[2] an-Nasaa’iy (4/22-23), at-Twabaraaniy (19/26) na al-Haakim (1/384).

[3] Ahmad (3/467).

[4] al-Bazzaar (857). al-Haythamiy amesema:

“Wapokezi wake ni wapokezi wa Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaa-id (3/8))

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 68-71
  • Imechapishwa: 16/08/2023