14. Baadhi ya hukumu kuhusu siku ya ´iyd II

Mtu anatakiwa kutahadhari kuumaliza mwezi huu mtukufu kwa kujipamba kwa mambo yasiyokuwa ya halali ikiwa ni pamoja na kunyoa ndevu, kuvaa nguo inayovuka kongo mbili za mguu na mengineyo aliyoharamisha Allaah. Bali analazimika kutubia tawbah ya kweli pengine akawa miongoni mwa wenye kukubaliwa.

Aende katika uwanja wa kuswalia ´iyd mapema ili awe karibu na imamu na fadhilah za kusubiri swalah. Aidha inapendeza kuja na njia hii na kurudi na njia nyingine. Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Inapokuwa siku ya ´iyd basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitofautisha njia.”[1]

Inapendeza ale tende kwa njia ya witiri – tatu, tano au zaidi – kutokana na maneno yake Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa harauki siku ya [´Iyd] al-Fitwr mpaka ale tende.”[2]

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Akizila witiri.”[3]

Hadiyth ya Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotangulia imefahamisha uwekwaji wa Shari´ah kwa wanawake kuhudhuria swalah ya ´iyd kwa sharti hayo yafanyike kwa njia ambayo kunaaminika wao kutopatwa na fitina au wao kuwafitinisha wengine. Kwa maana nyingine watoke hali ya kutojitia manukato, kutoonyesha mapambo na wenye kujiweka mbali na maeneo waliopo wanamme.

Ni lazima kwa muislamu akumbuke kule kukusanyika kwa waislamu kwa ajili ya kuswali ´iyd kukusanyika kwao katika uwanja mmoja, siku ya kufufuliwa na kulipwa, siku ambayo watu watasimama kwa ajili ya Mola wa walimwengu. Aidha akumbuke kule kushindana kwao katika mkusanyiko huu ambavyo watashindana pakubwa zaidi huko Aakhira. Allaah (Ta´ala) amesema:

انظُرْ كَيْفَ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَلَلآخِرَةُ أَكْبَرُ دَرَجَاتٍ وَأَكْبَرُ تَفْضِيلاً

”Angalia vipi tulivyowafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Aakhirah ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.”[4]

Ni lazima kwa muislamu atahadhari kutokana na kughafilika kumtaja Allaah na kumshukuru na azipambe nyakati zake kwa kumtii Allaah, kufanya mambo ya kheri na asizipoteze katika mambo ya pumbao na michezo, kama wanavofanya watu wengi wakati wa sasa. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.

[1] al-Bukhaariy (986).

[2] al-Bukhaariy (953).

[3] Fath-ul-Baariy (02/446).

[4] 17:21

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 08/03/2023