01. Ramadhaan na siku sita za Shawwaal – swawm ya mwaka mzima

01 – Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia [siku] sita za Shawwaal, basi anakuwa kama amefunga mwaka mzima.”[1]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth inajulisha juu ya fadhilah za kufunga siku sita za Shawwaal. Makusudio ya (الدهر) hapa ni mwaka. Kwa maana kwamba ni kama ambaye amefunga mwaka mzima. an-Nasaa´iy ameipokea ifuatavyo:

“Allaah hufanya jema moja mara kumi mfano wake. Mwezi inakuwa miezi kumi na kufunga siku sita baada ya Fitwr kunakamilisha mwaka.”[2]

Hii ni fadhilah ya Allaah kwa waja Wake kwa njia ya kwamba wanapata thawabu za kufunga mwaka mzima kwa njia isiyokuwa na uzito wowote. Hii ni moja ya hekima ya kufunga siku sita za Shawwaal. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Kwa hivyo mtu anatakiwa kufunga siku sita hizi ili aweze kufuzu kwa fadhilah hii kubwa. Alama ya kukubaliwa utiifu ni uunganishie kwa utiifu mwingine. Kufunga siku hizi ni dalili ya mtu kutaka kuendelea kufunga, kuipenda na kwamba haikumchosha na wala haikumlemea. Kufunga ni miongoni mwa matendo bora kabisa kama tulivyotangulia kusema.

Miongoni mwa matunda ya swawm inayopendeza – kama zilivyo ´ibaadah zingine za kujitolea – ni kwamba inafidia yale mapungufu na kasoro zinazopatikana katika kutekeleza ´ibaadah za faradhi. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusiana na swalah:

“Mola (Tabaarak wa T´ala) amesema: “Tazameni kama mja wangu anazo ´ibaadah za kujitolea ili ziweze kukamilisha yale mapungufu katika ´ibaadah za faradhi. Kisha itakuwa namna hiyo katika matendo yake mengine yaliyobakia.”[3]

Swawm inayopendeza inamwandaa pia muislamu kuzidi kupanda ngazi za kumkurubia Allaah na kupata mapenzi Yake. Kama ilivyo katika Hadiyth-ul-Qudsiy:

“Mja wangu hatojikurubisha Kwangu kwa mambo bora kuliko yale Niliyomfaradhishia. Mja wangu hatoacha kujikurubisha Kwangu kwa ´ibaadah za kujitolea mpaka nimpende… “[4]

[1] Muslim (164). Wanazuoni wamezungumzia juu ya Hadiyth hii kuishilia kwa Swahabah, jambo ambalo Imaam Ahmad pia amemili kwayo. Yametajwa hayo na Ibn Rajab katika al-Latwaaif”, uk. 256 na pia tazama “Risaalah” ya al-´Alaaiy” juu ya Hadiyth hii.

[2] an-Nasaa´iy katika ”al-Kabiyr” (03/239), Ibn Maajah (1715) na Ahmad (37/94). Ni Hadiyth Swahiyh. Ameisahihisha Imaam Abu Haatim katika ”al-´Ilal” nr. (745).

[3] Abu Daawuud (864), at-Tirmidhiy (413), an-Nasaa´iy (01/232-234), Ibn Maajah (1425) na Ahmad (13/278).

[4] al-Bukhaariy (6502).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 08/03/2023