13. Baadhi ya hukumu kuhusu siku ya ´iyd

09 – Ibn Abiy Shaybah amepokea kwa cheni ya wapokezi wake kupitia kwa az-Zuhriy ambaye amesimulia:

“Kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka siku ya Fitwr akileta Takbiyr mpaka anapofika uwanja wa kuswalia na mpaka anaposwali. Anapomaliza kuswali husimamisha Takbiyr.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi. Inatiliwa nguvu na Hadiyth zingine[1].

Hadiyth inafahamisha kuwa imewekwa katika Shari´ah kuleta Takbiyr kwa sauti njiani wakati wa kwenda katika uwanja wa ´iyd na pia anapofika uwanja wa kuswalia mpaka kutaposwaliwa.

Allaah amewawekea waja Wake Shari´ah kuleta Takbiyr wakati wa kumaliza idadi ya siku za Ramadhaan kuanzia kuzama kwa jua usiku wa kuamkia ´iyd mpaka wakati wa swalah ya ´iyd. Amesema (Ta´ala):

وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa amekuongozeni na ili mpate kushukuru.”[2]

Namna yake ni kusema:

الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله والله أكبر، الله أكبر ولله الحمد

“Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa na himdi zote njema ni za Allaah.”

Allaah amewawekea waja Wake Shari´ah ya swalah ya ´iyd. Ni katika ukamilifu wa kumtaja Allaah (Ta´ala). Ni Sunnah ambayo muislamu hatakiwi kuiacha. Wako wanazuoni wenye kuona kuwa ni lazima. Dalili yao ni yale aliyopokea Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa nje siku ya ´iyd mbili wanawake vijana ambao ndio karibuni wametoka kukomaa, wanawake wenye hedhi na mabikira. Kuhusiana na wanawake wenye hedhi, wajitenge mbali na kuswali.”[3]

Kuamrishwa kutoka kunapelekea kulazimishwa kuswali kwa ambaye hana udhuru wowote. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaamrisha wanawake, basi wanamme wana haki zaidi ya kulazimishwa.

Wanamme wanatakiwa watoke kwenda kuswali ´iyd  wakiwa katika hali nzuri ya kujipamba kwa vitu vilivyohalalishwa, amevaa mavazi yake mazuri kabisa hali ya kumuigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Muswannaf (02/164) ya Ibn Abiy Shaybah. Tazama pia zingine zinazoitia nguvu katika ”Ahkaam-ul-´Iydayn”, uk. 110 ya al-Firyaabiy, Fath-ul-Baariy (06/104) ya Ibn Rajab.

[2] 02:185

[3] al-Bukhaariy (980) na Muslim (890).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 08/03/2023