2 – Miongoni mwa mambo muhimu ambayo tunatakiwa kuupokea mwezi wa Ramadhaan uliyobarikiwa ni sisi kuipokea kwa kutubia tawbah ya kweli kutokamana na kila dhambi na kosa. Sote ni wenye kukosea. Sote ni lazima tuwe tumefanya upungufu, kupindukia, kuchupa mpaka na kufanya upungufu katika baadhi ya mambo. Imepokelewa katika Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Kila binadamu ni mwenye kukosea na mbora ya wenye kukosea ni wale wenye kutubia.”[1]

Ni lazima mwanadamu awe na makosa na mapungufu. Lakini wabora wa wenye kukosea ni wale wenye kutubia.

Ramadhaan ni msimu mtukufu wa kutubia kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Ni watu wangapi walikuwa ni wenye kupindukia mipaka katika mambo yao, wakipoteza utiifu wa Mola Wao na wakiyaendea mambo mengi ambayo ni ya maovu, lakini wakati wakati walipoingiliwa na mwezi huu mtukufu nafsi zao zikayachangamkia mambo ya kheri, wakahisi ule umuhimu wa utiifu na kumwelekea Allaah na kukapatikana ndani ya nafsi zao majuto juu ya kuzembea kumtii Allaah. Mwishowe wakatubia kwa Allaah tawbah ya kweli. Ni watu wangapi ambao wametubia tawbah ya kweli ndani ya mwezi huu mtukufu na baadaye hawakurudi katika yale waliyokuwemo katika nyakati zao zilizotangulia katika maasi na kuchupa mpaka. Ikiwa yule anayechupa mpaka, anayepoteza na kufanya mapungufu kunako haki za Allaah nafsi yake haikuchangamkia kutubu kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) katika mfano wa kipindi hiki, ni lini basi moyo wake utatikisika? Ikiwa hisia zake hazitatikisika wakati kama huu, ni lini zitatikisika? Kwa ajili hii mwezi wa Ramadhaan ni msimu mtukufu miongoni mwa misimu ya kutubu kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa hivyo tuupokee mwezi huu kutubia kwa Allaah tawbah ya kweli kutokamana na kila dhambi na kosa.

Allaah haikubali tawbah kutoka kwa waja Wake isipokuwa pale inapokuwa ya kweli. Tawbah ya kweli ni lazima itimize sharti tatu:

1 – Kujutia kufanya madhambi.

2 – Kuazimia kutoyarejelea.

3 – Kujinasua nayo kikamilifu.

Kwa sharti hizi tatu Allaah anaikubali tawbah ya mja pindi anapotubia. Anatakiwa kujinasua na dhambi kikamilifu, azimie moyoni mwake kuwa hatoirejelea maishani na ajutie majuto makubwa juu ya kutumbukia kwake ndani ya dhambi hiyo. Tawbah ikitimiza sharti hizi basi inakubaliwa. Wanazuoni wameongeza juu ya sharti hizi nne sharti ya nne: ikiwa dhambi inahusiana na haki za wanadamu. Kwa mfano amechukua pesa kutoka kwa mtu, ameshambulia haki miongoni mwa haki zake na mfano wake, basi kumeshurutishwa kwa ambaye hiyo ndio hali yake sharti ya nne ambayo ni kurudisha haki hiyo kwa mwenye nayo. Allaah atuwafikishe sote kutubia tawbah ya kweli kutokamana na kila dhambi na kosa.

[1] at-Tirmidhiy (2499) na Ibn Maajah (4251) kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh). Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb” (3139).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 18-20
  • Imechapishwa: 14/04/2022