Endapo tutaelezea kheri za mwezi huu, sifa zake za kipekee, fadhilah zake na nafasi yake basi wakati utarefuka. Lakini hebu wacha tuzungumzie kidogo yale mambo yanayotakikana kwetu kuipokea Ramadhaan na namna gani tunatakiwa kuipokea. Nitamuorodheshea msomaji mtukufu baadhi ya nukta na ambazo ni muhimu zaidi:

1 –  Tunatakiwa kufurahikia mwezi huu pale unapoingia furaha kubwa na kufurahi kwa kufika kwake na uwe na nafasi na daraja ya juu kabisa moyoni mwake. Aidha tumshukuru Allaah kwa kule kututunuku kuufikia. Ni watu wangapi ambao wameshuhudia mwezi wa Ramadhaan uliyopita na miezi mingine ya kabla yake lakini muda wa wao kueshi umemalizika na hivyo hawakuuridiki mwezi huu. Walikuwa na shauku kuweza kuufikia. Hatujui pengine baadhi yetu tusiweze kuufikia na pengine baadhi yetu wakafikia baadhi yake. Kwa ajili hiyo muislamu anapaswa kupupia wakati Allaah anapomkirimu na akamneemesha kufikia mwezi huu basi apupie kumshukuru Allaah kwa kule kumtunuku kuweza kuufikia. Kule kuufikia mwezi wa Ramadhaan hali ya kuwa katika uzima, afya njema, amani na imani hapana shaka kwamba hiyo ni neema kubwa ambayo unatakiwa kuithamani na kutambua nafasi yake.

Miongoni mwa kushukuru neema za Allaah juu yako ikiwemo kufikia mwezi huu mtukufu ni wewe kupupia, kujipinda na kujitahidi katika kumtii Allaah ndani yake. Allaah amekufikisha na hivyo pupia kumtekelezea Allaah haki Yake kukiwemo kufunga, kusimama usiku, kumtii, kujiurubisha Kwake na kujiepusha na mambo ambayo Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameyaharamisha.

Ilikuwa ni miongoni mwa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati anapoona mwezi mwandamo wa mwezi wowote basi husema:

اللّهُمَّ أَهِلَّـهُ عَلَيْـنا بِالأمْـنِ وَالإيمـان، والسَّلامَـةِ والإسْلامِ، رَبُّنـا وَرَبُّكَ اللهُ

”Allaah ni mkubwa! Ee Allaah! Uanzishe kwetu kwa amani na imani, usalama na Uislamu, Mola wetu na Mola wako ni Allaah.”[1]

Allaah akikutunuku na ukaingia mwezi huu uliobarikiwa na ukaona mwezi mwandamo, basi omba kwa du´aa hii iliopokelewa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba wakati anapoona mwezi mwandamo katika kila mwezi. Ni du´aa tukufu ambayo unamwomba Mola Wako (Subhaanahu wa Ta´ala) akubariki ndani ya mwezi wako, akutunuku amani, imani, kukusalimisha na mambo ya shari na kutekeleza haki za Uislamu kwa njia inayomridhisha Mola Wako (Tabaarak wa Ta´ala). Hapana shaka kwamba kuingia kwako mwezi huu ni neema kubwa inayokupasa kumshukuru Allaah kwayo na kuithamani ipasavyo.

[1] at-Tirmidhiy (3451) na Ahmad (1397) kupitia kwa Twalhah bin ´Ubaydillaah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 14/04/2022