127. Waislamu hawavai nguo zilizochovywa kwenye manjano

Mavazi:

1 – ´Abdullaah bin ´Amr al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliniona nimevaa nguo mbili za manjano akasema: ”Hizi ni miongoni mwa nguo za makafiri. Hivyo, usizivae.”[1]

[1] Muslim, an-Nasaa’iy, al-Haakim, Ahmad na ar-Raamhurmuziy. al-Haakim amesema:

”Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Hata hivyo hawakuipokea.”

Amekosea aliposema kuwa Muslim hakuipokea.

Hadiyth hii inakataza kuvaa nguo ambazo ni maalum kwa makafiri. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ametoa sababu ya makatazo ya kuzivaa kwamba ni katika mavazi ya makafiri, pasi na kujali alikusudia kuwa mavazi hayo wanayahalalisha makafiri kwa kuburudika nayo duniani au wameyazowea. Ni kama ambavo alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Wanastarehe kwa vyombo vya dhahabu na vya fedha duniani, lakini ni vya waumini huko Aakhirah.”

Ndio maana wanazuoni wamefanya kutumia hariri na dhahabu na fedha ni katika kujifananisha na makafiri. al-Bukhaariy na Muslim wamesimulia kwamba Abu ´Uthmaan an-Nahdiy amesema:

”Wakati tulipokuwa Azerbaijan pamoja na ´Utbah bin Farqad, ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alitutumia barua akisema yafuatayo:

”Ee ´Utbah! Sio katika mapato ya baba yako wala si katika matapo ya mama yako. Washibishe waislamu katika kambi zao kama unavyojishibisha mwenyewe katika kambi yako. Nakutahadharisha na anasa, mavazi ya washirikina na nguo za hariri, kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza nguo za hariri isipokuwa kwa kiwango hichi – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyoosha kidole chake katikati na kidole chake cha shahada na akavikutanisha ili tuvione.”

Abu Bakr al-Khallaal amepokea kutoka kwa Muhammad bin Siyriyn aliyesimulia kuwa Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh) alifika kwenye nyumba na akaona ajali mbili: mitungi ya shaba na risasi. Akakataa kuingia kwa kusema: “Yeyote mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”

Imekuja katika tamko jingine:

”Akaona kitu katika mavazi ya wasiokuwa waarabu, akatoka nje na kusema: “Yeyote mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.” (Iqtidhwaa’-us-Swiraat al-Mustaqiym, uk. 57-58)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 183-184
  • Imechapishwa: 13/11/2023