127. Mwanamume wa Kiislamu kumuoa mwanamke wa Ahl-ul-Kitaab

Kuhusu mwanaume wa Kiislamu kumuoa dada wa kikafiri. Kafiri huyo akiwa sio Ahl-ul-Kitaab haitokuwa halali. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَنكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ حَتَّىٰ يُؤْمِنَّ

”Na wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini.” (al-Baqarah 02:221)

Isipokuwa tu katika Aayah hii kunavuliwa muislamu mwanaume kumuoa mwanamke wa Ahl-ul-Kitaab kwa dalili ya Aayah ya Suurah “al-Maaidah” pale aliposema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖوَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلَا مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ

”Leo mmehalalishiwa vizuri na chakula cha wale ambao walipewa Kitabu ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao na wanawake wenye heshima wenye kujilinda na machafu miongoni mwa waumini wanawake na wanawake wenye heshima wenye kujilinda na machafu miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu; mtakapowapa mahari yao mkafunga nao ndoa bila ya kufanya uhasharati wala kuwafanya hawara.” (al-Maidah 05:04-05)

Makusudio ya chakula hapa ni vichinjwa vyao. Allaah amemhalalishia mwanaume wa Kiislamu kumuoa mwanamke Muhswanah ambaye ni yule mwenye kuilinda heshima yake. Ama kuhusu mwanamke aliyeharibika katika heshima yake haijuzu kwa muislamu kumuoa. Ni mamoja mwanamke huyo ni kafiri au muislamu. Amesema (Ta´ala):

الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ ۚ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ

“Mwanamme mzinifu hafungi ndoa isipokuwa na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina na mwanamke mzinifu haolewi isipokuwa na mwanamme mzinifu au mshirikina – na yameharamishwa hayo kwa waumini.” (an-Nuur 24:03)

Kwa hivyo Allaah kahalalisha mwanaume wa Kiislamu kumuoa mwanamke kafiri kwa masharti mawili:

1- Awe ni mwenye kuilinda heshima yake. Sio mwasherati wala kuwafanya hawara.

2- Awe ni mwanamke wa Ahl-ul-Kitaab; mwanamke myahudi au mnaswara.

Katika hali hii inafaa kwa muislamu kumuoa.

Lakini inaweza kusemwa: ni jambo lenye kujulikana ya kwamba baina ya mume na mke kunakuwa mapenzi. Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَة

”Amekujaalieni baina yenu mapenzi na huruma.” (ar-Ruum 30:21)

Vipi basi atamuoa mwanamke wa Ahl-ul-Kitaab ambaye ni kafiri na akampenda? Inajuzu kwa muislamu kumpenda mwanamke wa kikafiri? Pamoja na kwamba amesema (Ta´ala):

لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ

“Msifanye adui Wangu na adui wenu kuwa wapenzi mkiwapa mapenzi.” (al-Mumtahinah 60:01)

Jawabu ni kwamba mapenzi ya kindoa hakuna neno ndani yake. Ama mapenzi ya kidini hayajuzu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 164-165
  • Imechapishwa: 28/02/2019