12. Qur-aan na Sunnah vinatosha

Allaah (Ta´ala) amemkemea ambaye hakutosheka na Wahy Wake na akasema:

أَوَلَمْ يَكْفِهِمْ أَنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَرَحْمَةً وَذِكْرَىٰ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Je, haikuwatosheleza kwamba hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu wanachosomewa? Hakika katika hayo bila shaka kuna rehema na ukumbusho kwa watu wanaoamini.”[1]

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Kwa hakika katika visa vyao kuna mazingatio kwa wenye akili. Haikuwa [Qur-aan] hadithi zinazotungwa, lakini ni sadikisho la [vitabu] vya kabla yake na pambanuo ya waziwazi ya kila kitu na ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.”[2]

كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَى صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ

”Kitabu Tumekiteremsha kwako ili uwatoe watu katika viza kuwaingiza katika nuru kwa idhini ya Mola wao, waelekee katika njia ya Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[3]

وَلَقَدْ جِئْنَاهُم بِكِتَابٍ فَصَّلْنَاهُ عَلَىٰ عِلْمٍ هُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Kwa hakika Tumewaletea Kitabu tulichokipambanua waziwazi kwa ujuzi; na ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.”[4]

أَفَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْتَغِي حَكَمًا وَهُوَ الَّذِي أَنزَلَ إِلَيْكُمُ الْكِتَابَ مُفَصَّلًا

“Je, nitafute hakimu asiyekuwa Allaah Naye ndiye Kakuteremshieni Kitabu kilichopambanuliwa waziwazi?”[5]

Kuna Aayah nyingi mfano wa hizo ndani ya Qur-aan. Hiyo inafahamisha kuwa Allaah amebainisha dini yote na ameweka wazi njia ya uongofu. Qur-aan inamtosheleza yule mwenye kuifuata, haitaji kitu kingine. Ni lazima kuifuata na si kitu kingine[6]. ´Abdullaah bin ´Umar (RadhiyaAllaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hajapatapo kumtuma Mtume yeyote isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake kuwajulisha Ummah wake ya kheri anayojua juu yao na kuwakataza ya shari anayoyajua juu yao.”[7]

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi watu! Hakuna chochote kinachokuwekeni karibu na Pepo na kinachokuweni mbali na Moto isipokuwa nimekuamrisheni nacho, na hakuna chochote kinachokuwekeni mbali na Pepo na kinachokuweni mbali na Pepo isipokuwa nimekukatazeni nacho.”[8]

[1] 29:51

[2] 12:111

[3] 14:1

[4] 7:52

[5] 6:114

[6] Tazama ”Dar’ Ta´aaridhw-il-´Aql wan-Naql” (10/304) ya Ibn Taymiyyah.

[7] Muslim (1844).

[8] al-Haakim (2/4), al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan” (3/1458) na Sharh-us-Sunnah (14/303-305) ya al-Baghawiy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 03/05/2023