12. Kula na masikini na wagonjwa

49 – Muhammad amesema: Khaalid bin ´Amr al-Umawiy ametuhadithia: Nilimsikia Khulayd bin Da´laj akitaja kwamba Muhammad bin Waasiy´ amesema:

”Mwenye kula kidogo hufahamu na kuwafanya wengine wakafahamu, akasafika na kutakaswa. Chakula kingi humlemea mlaji wake, matokeo yake akazuilika kutokana na mengi anayotaka kuyafikia.”

50 – Yahyaa bin Yuusuf az-Zammiy ametuhadithia: Abul-Maliyh ametuhadithia, kutoka kwa Maymuun bin Mihraan, kutoka kwa Naafiy´, ambaye amesema:

”Kila jioni Ibn ´Umar alikuwa akiwakusanya familia yake kwenye sahani. Akija mwombaji, basi anampa sehemu yake katika uji. Baada ya kuliwa kila kitu kilichokuwemo kwenye sahani, anarudi. Ikiwa nimekula kitu kutoka humo, basi Ibn ´Umar naye amekila. Kisha anaamka asubuhi hali ya kuwa amefunga.”

51 – Yahyaa bin Yuusuf ametuhadithia: Abul-Maliyh ametuhadithia, kutoka kwa Maymuun, ambaye ameeleza:

”Mmoja katika watoto wa Ibn ´Umar alimjia na kusema: ”Nivishe kikoi.” Kikoi chake kilikuwa kirefu. Akasema: ”Nenda ukifupishe kisha kiunganishe kwa kukishona. Kitakutosha. Naapa kwa Allaah! Naona kuwa mtayafanya yale ambayo Allaah amekuruzukuni ndani ya matumbo yenu na kwenye ngozi zenu, lakini mnawapuuza wajane, masikini na mayatima wenu.”

52 – Muhammad bin Yahyaa bin Abiy Haatim ametuhadithia: ´Attwaab bin Ziyaad ametuhadithia: ´Abdullaah bin al-Mubaarak ametuhadithia: Ibn Lahiy´ah ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan bin Nawfal al-Asdiy, aliyesimulia kuwa Swafiyyah bint Abiy ´Ubayd amesema:

”Sikumuona ameshiba ili niseme kuwa ameshiba.” Anamkusudia Ibn ´Umar. Kisha akasema: ”Nilipoona jambo hilo, na alikuwa na mayatima wawili, nilimpikia kitu. Ndipo akanambia niwaite na akala pamoja nao. Waliposimama, nikamletea chakula zaidi. Ndipo akanambia nimwite fulani na fulani. Nikamwambia kuwa wamelala na wameshiba. Akasema: ”Niitie baadhi ya watu waliokuwa wakilala chini ya paa (أَهْلِ الصُّفَّةِ). Wakaitwa masikini na wakala naye.” 

53 – Muhammad bin Yahyaa ametuhadithia: Muhammad bin Ja´far al-Madaainiy ametuhadithia: Shu´bah ametukhabarisha, kutoka kwa ´Uthmaan bin Saliytw, ambaye ameeleza:

”Ibn ´Umar alikuwa akiwaita watu wenye ukoma, akila nao na akisema: ”Pengine katika hawa kukawepo Malaika siku ya Qiyaamah.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 19/06/2023