11. Usilale hali ya kuwa umeshiba

41 – Khaalid bin Khidaash ametuhadithia: al-Mu´allaa al-Warraaq ametuhadithia: Nilimsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Nilichanganya unga wangu na majivu na nikadhoofika kutokana na swalah. Ningelikuwa na nguvu ya kuswali basi nisingekula chakula kingine zaidi yake.”

42 – Khaalid ametuhadithia: al-Mu´allaa al-Warraaq ametuhadithia: Abu ´Ubaydah al-Khawwaasw amesema:

”Kifo chako kiko katika shibe yako na bahati yako iko katika njaa yako. Ikiwa umeshiba [tupu] na ukalala, basi adui anaweza kumakinika kwako. Lakini unapokuwa na njaa, basi unakuwa makini juu ya adui.”

43 – ´Abdullaah bin ´Iysaa at-Twafaawiy ametuhadithia: ´Abdullaah ash-Shahhaam ametuhadithia: Maalik bin Diynaar amesema:

”Kwa muda wa asubuhi arobaini nilikula chakula cha kubana. Isingekuwa kwamba nachelea kudhoofika, basi ningelazimiana na jambo hilo.”

44 – Muhammad bin ´Umar bin ´Aliy al-Muqaddimiy amenihadithia: Nilimsikia Yuusuf bin ´Atwiyyah bin Baab as-Swaffaar: Nilimsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Ingelikuwa majivu yanaingia kooni mwangu, basi ningeyala.”

45 – Haaruun bin ´Abdillaah ametuhadithia: Sayyaar ametuhadithia: ´Uthmaan bin Ibraahiym, mmoja katika marafiki zake Maalik bin Diynaar, ametuhadithia:

”Nilimsikia Maalik akimwambia mmoja katika ndugu zake: ”Natamani mkate laini na mnene kwa mtindi.” Bwana yule akaondoka na kumletea navyo. Akawa akavitazama na kusema: ”Mimi nimekutamani tangu miaka arobaini iliyopita na daima nimekushinda – unataka kunishinda hivi sasa? Viondoshe hapa kwangu.” Akakataa kuvila.

46 – Muhammad bin al-Husayn amesema: Khaalid bin Yaziyd at-Twabiyb ametuhadithia: Khaazim bin al-Husayn ametuhadithia: Nilimsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Unalipenda tumbo lako zaidi kuliko dini yako? Je, unalitanguliza mbele tumbo lako kuliko nafsi yako? Hebu wazia umelijaza chakula kizuri na kinywaji kitamu zaidi – tazama ni nini [tupu].”

47 – Haaruun bin ´Abdillaah ametuhadithia: Sayyaar ametuhadithia: Ja´far ametuhadithia: Nilimsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Ni nani yuko katika kikao chenu hiki? Naapa kwa Allaah! Hapo sijaonja tende ambayo haijakomaa, tende tosa wala tende kavu. Ni kipi kimepungua kwangu na kukunyanyueni nyinyi?”

48 – Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Daawuud bin Muhabbar ametuhadithia: ´Abdul-Waahid bin Ziyaad ametuhadithia: Nilimsikia Maalik akimwambia Hawshab:

”Ee Abu Bishr! Yahifadhi kutoka kwangu mambo mawili: usilale hali ya kuwa umeshiba na kiache chakula hali ya kuwa unakitamani.” Hawshab akasema: ”Ee Abu Yahyaa! Hayo ni maelekezo ya mapishi ya madaktari wa ulimwenguni.” Muhammad bin Waasiy´ akayasikia maneno yao akasema: ”Ndio, na ni maelekezo ya mapishi ya njia ya kwenda Aakhirah.” Ndipo Maalik akasema: ”Hapana, ni ya Aakhirah na ulimwenguni.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 19/06/2023