10. Kwa sababu ulikuwa unafunga duniani

38 – Haaruun bin ´Abdillaah ametuhadithia: Sayyaar ametuhadithia: Ja´far ametuhadithia: Yuusuf bin Ya´quub al-Hanafiy ametuhadithia:

”Tumefikiwa na khabari kwamba Allaah (´Azza wa Jall) atawaambia mawalii Wake siku ya Qiyaamah: ”Ee mawalii Wangu! Mara nyingi nilikuoneni mkiinamisha macho chini duniani, midomo yenu ikawa mikavu kutokana na kiu na yakanguruma matumbo yenu. Sasa kunyweni kwa pamoja kutoka katika kikombe hiki. Hii leo kuleni:

وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ

”… wa kunyweni kwa furaha kwa yale mliyoyatanguliza katika siku nyingi zilopita.”[1]

39 – Abu Ja´far al-Kindiy ametuhadithia: Muhammad bin Swabiyh ametuhadithia: Sa´iyd bin Bashiyr ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”Wakati ambapo walii wa Allaah atakuwa ameegemea na mkewe wa Peponi kwenye mto wa asali, atampa kikombe na kusema: ”Uzuri uliyoje wa maisha! Unajua, ee kipenzi cha Allaah, ni lini Mola wangu aliniozesha kwako?” Atasema: ”Sijui.” Ndipo mwanamke huyo atasema: ”Allaah alikutazama katika siku ya kiangazi na siku ndefu ya majira ya joto wakati ulipokuwa na kiu, na Akajifakharisha mbele ya Malaika Wake na kusema: ”Mwangalieni mja Wangu! Amemwacha mke wake, matamanio yake, ladha yake, chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu na kwa ajili ya kutaka thawabu Zangu. Nakushuhudisheni kwamba nimemsamehe!” Basi akakusamehe siku hiyo na akaniozesha wewe.”

40 – Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Buhluul ametuhadithia, kutoka kwa Bishr bin Mansuur, kutoka kwa Thawr, kutoka kwa Khaalid bin Ma´daan, ambaye amesema:

”Nilisoma kwenye kitabu kimoja: ”Ifanye nafsi yako kuwa na njaa na uchi, ili ipate kamuona Allaah.”

[1] 69:24

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 19/06/2023