112. Maswahabah wanatakiwa kuombewa du´aa na kusifiwa

Wala haijuzu kwa yeyote kujishughulisha na magomvi ya Maswahabah. Mlango huu unatakiwa kufungwa kwa ajili ya kuonyesha heshima kwao. Maswahabah wanazo fadhilah na matendo matukufu ambayo kwayo Allaah anasamehe kule kuteleza kwao. Hapo ni pale ambapo makosa hayo yatathibiti. Licha ya kwamba mengi yanayosemwa juu yao ni uongo. Allaah (Ta´ala) amesema kuwahusu:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao ni wenye kusema: “Mola wetu!Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini – Mola wetu! Hakika ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye mioyo na ndimi salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Yapo mambo matatu kuhusu Maswahabah:

1 – Wanatakiwa kuombewa du´aa.

2 – Wanatakiwa wasifiwe.

3 – Mioyo inatakiwa kusafika kutokamana na kuwachukia na ndimi kutokamana na kuwatukana, lakini hayo ni kinyume na wale wanaowalaani, wanawatusi na kutafuta kasoro zao. Kwa kufanya hivo wanaenda kinyume na amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 59:10

[2] al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 12

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 06/09/2021