65. Mwenye busara na kuwapa swadaqah wahitaji

1 – Jaabir amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajapatapo hata siku moja kuombwa kitu akasema hapana na wala hajapatapo hata siku moja kupiga kwa mkono wake.”

2 – Mimi napendekeza kwa kila mtu kuwa na tabia za juu na kuacha kuwarudisha nyuma waombaji. Ni bora kutokuwa na pesa kuliko kukosa tabia njema.

3 – Mtu huru wa kweli ni yule aliyeachiliwa huru kwa maadili mazuri. Mtumwa mbaya ni yule aliyefanywa mtumwa kwa maadili maovu. Miongoni mwa zawadi bora anazokwenda nazo mtu huko Aakhirah ni sifa nzuri.

4 – Yuusuf bin Asbaatw amesema:

“Tangu ulimwengu uumbwe pesa haijakuwa na faida kubwa kama ilivyo hii leo.”

5 – ´Ubaydullaah bin Ziyaad bin Dhwibyaan amesema:

“Nilikuwa na mjomba kutoka katika kabila la Kalb. Alikuwa akinambia: “Kuwa na hima! Hakika kuwa na hima ni nusu ya muruwa.”

6 – Abu Sulaymaan adh-Dhwabbiy amesema:

“Kasiri ya Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ilikuwa na milango minane. Pasi na kujali mwombaji atakuja kupitia wapi, anapewa.”

7 – Sa´iyd bin ´Abdil-´Aziyz amesema:

“al-Hasan bin ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alimsikia bwana mmoja pambizoni mwake akimwomba Allaah du´aa ampe dirhamu 10.000. Akaondoka na akamtumia mjumbe ampe kiwango hicho.”

8 – Abu Sa´iyd amesimulia kupitia kwa mwalimu wake aliyesema:

“Nilimuona Ibn-ul-Mubaarak akiuma meno mkono wa mtumishi wake. Nikamwambia: “Unauma meno mkono wa mtumishi wako?” Akasema: “Ni mara ngapi nimeshamwambia asimuhesabilie pesa mwombaji? Wape mgumi ikiwa na sarafu!”

9 – Ni wajibu kwa mwenye busara kuwapa wenzake na awatendee wema. Anatakiwa kuanza na wale ambao imelazimika zaidi kuwatendea wema kisha wanaowafuatia. Anatakiwa aanze na watu wa nyumbani kwake, kisha ndugu zake, majirani zake na kadhalika. Ahakikishe amewapa kipaumbele watu wa dini na wanazuoni.

10 – Mwenye busara huwapa wengine kabla hajaombwa. Ni bora kuanza kufanya kitendo hicho kuliko kulipiza wema. Ni bora kujizuia kuomba kuliko kutoa. Swadaqah ni nzuri pale inapokamilishwa na baadaye ikaendelea. Mwisho mzuri unasafisha mwanzo. Ni bora kutoa baada ya kwamba mtu alikuwa hatoi kuliko kuzuia baada ya kwamba mtu alikuwa anatoa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 252-258
  • Imechapishwa: 26/09/2021