113. Viongozi wa waislamu wanatakiwa kutiiwa

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Viongozi wa waislamu katika watawala na wanachuoni wanatakiwa kutiiwa.

MAELEZO

Hili ni miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wanachuoni wamelifanyia kazi katika katika vitabu vyao kuhusu ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Watawala wa waislamu wanatakiwa kusikilizwa na kutiiwa. Jambo hilo linapelekea katika manufaa na kuzuia madhara. Waislamu wanapaswa kukusanyika juu ya kumcha Allaah na kutendea kazi Shari´ah Yake. Amesema (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[1]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana.”[2]

Kwa hivyo waislamu wanapaswa kuwa na umoja; wasitofautiane. Waislamu hawawezi kukusanyika pasi na uongozi na utawala. Sambamba na hilo uongozi hauwepo pasi na kusikiliza na kutii. Allaah (Subhnaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[3]

Ametaja (Subhaanahu wa Ta´ala) kwamba utiifu unakuwa kwa mambo matatu:

1 – Allaah (´Azza wa Jall).

2 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

3 – Wale wenye mamlaka, bi maana viongozi na wanachuoni.

Manufaa ya utiifu na usikizi unarudi kwa watu wote. Mambo hujengeka, jamii yao inapata nguvu na adui wao anakuwa na heshima. Haya ndio yaliyoamrishwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakuusieni kumcha Allaah, na kusikiliza na kutii hata kama atatawalia juu yenu mja. Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu. Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu.”[4]

Huu ndio wasia wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Ummah wake. Pia ndio jambo alilousia Allaah pale aliposema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[5]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi; mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[6]

Kurejea kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunalengwa kurudi katika Qur-aan na Sunnah kupitia kwa wanachuoni. Kwa sababu wanachuoni ndio wenye mamlaka inapokuja katika elimu, viongozi ni wenye mamlaka kwenye mikakati ya siasa. Waislamu wanahitajia elimu na siasa. Mambo ya elimu yanasimamiwa na wanachuoni na mambo ya siasa yanasimamiwa na viongozi wa waislamu. Mambo ya waislamu hayanyooki isipokuwa kwa hayo mawili, pasi na kujali zama na mahali. Mambo hayanyooki kwa watu kuwatukana, kuwadharau, kutafuta aibu zao na kuyaanika mbele za watu hadharani. Mambo kama hayo yanasababisha kufanywa uasi dhidi yao, kuasiwa na kuleta mpasuko. Pindi mtawala anapofanya kosa basi anatakiwa kunasihiwa kwa siri kati ya mtoa nasaha na msihiwa.

[1] 03:103

[2] 03:105

[3] 4:59

[4] Ahmad (4/287), Abu Daawuud (4753), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (42). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (131).

[5] 03:103

[6] 04:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 06/09/2021