114. Ni lazima kuwa na utambuzi juu yaa mfumo wa Salaf

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Salaf wanatakiwa kufuatwa, kuyatendea kazi mapokezi yao na kuwaombea msamaha.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwafuata Salaf. Salaf ni Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wale waliowafuata mfumo wao kwa wema hadi siku ya Qiyaamah. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mayahudi wamegawanyika katika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika katika makundi sabini na mbili. Na Ummah huu utakuja kugawanyika katika makundi sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Wakasema: “Ni kina nani hao, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wenye kufuata yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ni mkusanyiko.”

Hawa ndio kundi lililookoka.

Kujinasibisha na Salaf na madhehebu yao kunahitajia elim juu ya ´Aqiydah na mfumo wa Salaf. Haitoshi mtu akadai tu kuwa yeye anafuata mfumo wa Salaf bila ya kuwa na elimu juu yao. Pengine akalipwa thawabu kutokana na nia na makusudio yake, lakini haitoshi. Ni lazima kwa mtu kujua yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah walikuwa wakiamini. Ndio maana Allaah (Jalla wa ´Alaa) akasema:

وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“… na wale waliowafuata kwa wema… “[2]

Bi maana kwa kumairi. Haiwezekani mtu akafikia hilo isipokuwa mpaka awe na utambuzi juu ya mfumo wao na yale waliyomo ili kule kujinasibisha kwake nao kuwe sahihi. Jengine ni kwamba haitoshi kule kujinasibisha peke yake pasi na kuwa na utambuzi juu ya mfumo wao. Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni wakayataja haya katika vitabu vinavyozungumzia ´Aqiydah. Ni jambo linalohusu misingi katika kitabu hiki, “al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah” cha at-Twahaawiy, “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” cha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na vyenginevyo. Wanachuoni wanalitaja hili katika vitabu vyao vya ´Aqiydah kwa ajili ya kutilia mkazo shani yake. Maudhui haya ni makubwa na mfumo ni wenye kunyooka. Ummah haurekebiki isipokuwa kwao. Imaam Maalik amesema:

“Hautotengemaa mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyoufanya kutengemaa wa mwanzo wao.”

Ni jambo zuri zile karne za mwisho zilizokuja kile kitendo cha kuwapenda Salaf na kupenda kuwaigiliza, lakini ni lazima kwao wasome ´Aqiydah na mfumo wao ili wayatambue kwa ujuzi na kushikamana nayo. Kwa sababu wako watu ambao wanawagumzisha waislamu mambo mbalimbali na kuyanasibisha na mfumo na matendo ya Salaf. Lengo lao ni kuwapotosha. Lakini mfumo wa Salaf uko wazi, umeandikwa na unasomeshwa na kwa ajili hiyo watu warejee kwao. Unatakiwa kufuatwa na kutekelezwa ili Ummah urekebike na itengemae hali yake.

[1] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[2] 09:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 86-88
  • Imechapishwa: 06/09/2021