11. Vifo vya kushtukiza kwa watumiaji wa pombe

Kwa hivyo tubuni juu ya madhambi yote. Pengine kifo kikakutokeeni ghafla pasi na kutubia na hivyo mtu katika hali ya kukata roho akawa miongoni mwa waliokula khasara. Imekwishatangulia kwamba matishio yanamgusa yule ambaye hakutubia. Imekuja katika Hadiyth ya Abu Hurayrah:

“Hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini. Baada ya hapo upo uwezekano wa kutubia.”[1]

Alikuweko mtu mmoja chapombe kutoka katika Naaswibiyn kwa jina Abu ´Amr. Usiku mmoja akanywa kisha baada ya hapo akalala ambapo akaamka katikati ya usiku akiwa na woga. Akasema: “Nimejiwa na mtu usingizini akanambia:

Hali yako ni ya khatari, ee Abu ´Amr

pamoja na hivyo umeishikilia pombe

Unakunywa mvinyo waziwazi kweupee na

yamekuchukua mafuriko pasi na wewe kujua

Kisha akalala. Ilipofika mida ya alfajiri akafa kifo cha ghafla[2].

Kuna mwingine alikunywa mpaka akalewa na akachukuliwa na usingizi mpaka ´Ishaa. Mke wake, ambaye alikuwa binamu yake, alikuwa mtu wa dini na alijaribu kumuamsha kwa ajili ya swalah. Baada ya majaribio mengi akakasirishwa na akaapa kwamba amemtaliki milele endapo ataacha swalah siku tatu zinazokuja huko mbele. Kulipokucha akachanganyikiwa kumtaliki binamu yake. Kwa ajili ya kutimiza kiapo chake hakuswali kwa muda wa siku mbili. Baada ya hapo akagonjweka na kufa. Baadhi wakasoma mashairi kwa ajili ya tukio hili:

Umejiaminisha, ee mlevi?

Hujui kuwa kifo kinaweza kukutokea ghafla kipindi cha ulevi wako

na hivyo ukawa ni mafunzo kwa watu wengine

na ukakutana na Allaah ukiwa na viumbe waovu kabisa

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu.”[3]

Imekuja katika Hadiyth:

“Majuto ni tawbah.”[4]

Kwa hiyo ni lazima kujutia, kujinasua na kuazimia kikamilifu kutorudi kufanya hivo. Kuhusu ambaye ataazimia kurudi, ingawa ni baada ya kipindi fulani, hazingatiwi kuwa ni mwenye kutubia. Ibn-ul-Mubaarak aliulizwa tafsiri ya ni nani mnywaji pombe ambapo akajibu:

“Ni yule anayekunywa leo kisha hanywi tena isipokuwa baada ya miaka thelathini na anafikiri kuinywa haraka iwezekano pale tu atapoipata.”

[1] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[2] al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan” (5610).

[3] 49:11

[4] Ibn Maajah (4252).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 23-25
  • Imechapishwa: 26/07/2020