11. Swahabah wa kike aliyepaka rangi mashavu yake

Hadiyth ya mwanamke iliopo kwa Abu Daawuud ni dalili ya wazi juu ya kwamba inafaa kwa mwanamke kuonyesha uso na mikono yake endapo cheni ya wapokezi isingelikuwa na upungufu. Hata hivyo mtu anaweza kusema kuwa inatiliwa nguvu na njia zake nyingi. al-Bayhaqiy ameitia nguvu kutokana na sababu hiyo. Kwa ajili hiyo inafaa kuwa ni dalili kwamba kitendo hicho kinafaa. Hadiyth inatiliwa nguvu vilevile na kitendo cha wanawake wengi katika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao walikuwa wakionyesha uso na mikono yao mbele yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na yeye kuwakemea juu ya hilo. Zipo dalili nyingi juu ya hilo. Hapa tutaorodhesha baadhi ya zile ambazo nakumbuka:

1 – Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Nilishuhudia pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah siku ya ´iyd. Akaanza kuswali kabla ya kutoa Khutbah pasi na kuadhini wala kukimu. Kisha akasimama hali ya kumuegemea Bilaal ambapo akaamrisha kumcha Allaah na akahimiza kumtii; akawawaidhi na kuwakumbusha watu. Kisha akaondoka kwenda kwa wanawake akawawaidhi na kuwakumbusha. Akasema: ”Enyi wanawake! Toeni swadaqah! Hakika wengi wenu ni kuni za Motoni.”Mwanamke mmoja aliyekuwa amekaa katikati yao na ambaye alikuwa amejipaka rangi mashavu yake akasimama na kusema: ”Kwa nini, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa sababu nyinyi mnalalamika sana na ni wakosefu wa shukurani kwa waume zenu.”Ndipo wakaanza kutoa swadaqah vito vyao; wakawa wanamrushia Bilaal hereni na pete zao.”[1]

[1] Muslim (3/19), an-Nasaa’iy (1/233), ad-Daarimiy (1/377), Ibn Khuzaymah (1460), al-Bayhaqiy (3/296) na (3/300) na Ahmad (3/318).

Hadiyth ni dalili ya wazi na tumeitaja kwa lengo hilo. Vinginevyo angewezaje msimuliaji kumweleza mwanamke yule kwamba alikuwa amepaka rangi mashavu yake?

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 57-60
  • Imechapishwa: 05/09/2023