11. Subira juu ya kuharibika kwa mimba

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wazazi wa mimba iliyoharibika wakiingia Motoni, basi itamuomba Mola wake (´Azza wa Jall) kwa king´ang´anizi, kutasemwa: “Ee mimba iliyoharibika unayemuomba Mola wake! Waingize wazazi wako Peponi!” Itawavuta kwa kitovu chake mpaka iwaingize Peponi.”[1]

Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake! Hakika mimba iliyoharibika itamvuta mama yake kwa kitovu chake kuingia Peponi endapo atatarajia malipo.”[2]

Zote mbili amezipokea Ibn Maajah peke yake. Hata hivyo ´Abd bin Humayd amepokea Hadiyth ya Mu´aadh ndefu ambapo Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakuna waislamu wawili wanaofisha watoto watatu, isipokuwa Allaah atawaingiza wawili wake Peponi kutokana na fadhilah za rehema Yake juu yao.” Wakasema: “Vipi kuhusu wawili, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Na wawili.” Wakasema: “Na mmoja, ee Mtume wa Allaah?”Akasema: “Hakika mimba iliyoharibika itamvuta mama yake kwa kitovu chake kuingia Peponi.”[3]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimba iliyoharibika kabla yangu inapendeza zaidi kwangu kuliko shujaa ninayemwacha nyuma yangu.”[4]

Ameipokea Ibn Maajah.

Layth bin Sulaym amesimulia kutoka kwa Sa´iyd, kutoka kwa Humayd bin ´Abdir-Rahmaan al-Humaydiy aliyesimulia kuwa bwana mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Mtume wa Allaah! Nini ninachopata mimi juu ya watoto wangu?” Akasema: “Wale waliokutangulia mbele ya haki katika wao.” Akasema: “Vipi wale ninaowaacha nyuma yangu?” Akasema: “Utapata katika wao yale Mudhwar aliyopata kwa watoto wake.”Humayd akasema: “Mimba iliyoharibika kabla yangu inapendeza zaidi kwangu kuliko wanamme mia moja walio na ngao.”

Abu Hassaan Muslim bin Khaalid al-A´raj amesema:

“ Nilisema kumwambia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh): “Nimefiwa na wanangu wawili. Hujasikia chochote kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambacho kitatufurahisha baada ya wafu wetu?” Akasema: “Ndio: Wadogo wao ndio mabuu ya Peponi. Watakutana na baba zao – au wazazi wao – wawashike nguo zao – au mkono wake – kama ambavo mimi nashika pindo la vazi lako hili na hawatoliacha mpaka pale ambapo Allaah atawaingiza wao na wazazi wao Peponi.”[5]

Imekuja katika upokezi mwingine “wanapiga mbizi katika mito ya Peponi”. Kwa maana nyingine wakicheza ndani ya mito ya Peponi.

[1] Ibn Maajah (1610). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (316).

[2] Ibn Maajah (1609). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (1315).

[3] Ahmad (5/241).

[4] Ibn Maajah (1607). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (315).

[5] Muslim (2635), al-Bukhaariy katika “al-Adab al-Mufrad” (1/231) na Ahmad (2/488).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 61-67
  • Imechapishwa: 14/08/2023