Mara nyingi nimetahadharisha malazimisho, kuzungumza juu ya watu wengine pasi na elimu, kuyapotosha maneno yao, kuongeza au kupunguza au kufasiri kimakosa. Nimeyazungumzia hayo mara nyingi kwenye msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baadhi ya mihadhara yangu mingine. Aliyefahamu kwa maneno yangu haya kuwa namkusudia yeyote katika ndugu zangu au waalimu waheshimiwa basi ni mwongo mbaya na mzushi na anayenisemea pasi na elimu. Sintomsamehe kwa jambo hilo. Namshtaki kwa Allaah (´Azza wa Jall). Nitaomba du´aa dhidi yake kwa kuyapotosha maneno yangu na kusema kuwa nawakusudia baadhi ya wanazuoni wetu waheshimiwa kama vile mwalimu wetu Shaykh Rabiy´ (Hafidhwahu Allaah) au mwingine katika wanazuoni wetu. Mwenye kusema kuwa nimewakusudia wao ni mwongo mbaya. Haya ndio katika malazimisho ambayo nimetahadharisha kwayo. Muhadhara wangu wa mwisho nimetoa Maroko yamekengeushwa. Baadhi ya wapumbavu wameyachukulia kuwa namlenga fulani na fulani. Wakati ninapoita katika hekima, ustadi, kuhakikisha, ukweli, ukweli katika kunakili maneno, kutofanya malazimisho au kufanya uangalifu katika kuwahukumu wengine, nafanya hivo kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah kwa njia ya mwongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na bali maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall) aliposema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuwa makini na kuhakikisha, jambo ambalo limetajwa katika Aayah nyingi za Qur-aan na Hadiyth. Kwa hivyo mwenye kudai kuwa kwa maneno haya namkusudia yeyote katika waalimu zetu, ndugu zangu au wanafunzi – mwenye kuyapotosha maneno yangu – basi mimi sintomsamehe. Bali nitamuombea du´aa mbaya mwishoni mwa usiku. Hii ndio tabia ya wale watu wenye papara. Ni kama mfano wa wale watu wanaowauliza maswali wanazuoni wetu wakubwa kama vile Shaykh Swaalih al-Fawzaan, Muftiy [´Abdul-´Aziyz Aal ash-Shaykh] au wengine katika wanazuoni wetu. Udhahiri wa swali ni mzuri. Kisha baada ya hapo wanalieneza na kuliandikia mabango juu ya kwamba Shaykh fulani anamraddi mtu fulani. Haya ndio ambayo mimi nayakemea na daima nayatahadharisha. Wanatakiwa kujishughulisha na elimu, wajiepushe na tashwishi na watubie kwa Allaah (´Azza wa Jall) kutokana na makengeusho haya na malazimisho haya. Yule mwenye kudai kuwa pale ninapotahadharisha nawakusudia ndugu zangu katika Salafiyyuun basi ni mwongo mbaya. Naweza kuwanasihi ndugu zangu kuwa na hekima, kuhakikisha au umakini katika kunukuu, lakini mtu akifahamu kimakosa, kama zinavofanya baadhi ya tovuti zinazotumia fursa maneno ya baadhi ya wanazuoni ili kuyapachika kwa nia mbaya kwa wanazuoni wengine na kueneza maneno yanayofahamika kuwa fulani anamlenga fulani, ni jambo tunalitambua tangu hapo kale. Wameyakengeusha maeneno ya Shaykh wetu Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) wakati alipowashauri walinganizi kuwa na hekima, kulingania kwa maneno mazuri, kujadili kwa njia bora zaidi, kuhakikisha na kutokuwa na haraka. Ndipo wakasema kuwa anawakusudia wanazuoni wa Madiynah. Waliyasema hayo tangu hapo zamani. Wale wanaosema kuwa nawakusudia ndugu zangu Salafiyyuun ni waongo. Wanavuka mipaka yao. Nitawaombea du´aa mbaya mwishoni mwa usiku. Sintowasamehe.

Waambie watu hao ambao wanadai kuwa nimemkusudia fulani na fulani wamche Allaah. Ni lazima kwao kumcha Allaah na wasiwatie maneno kwenye mdomo ndugu zao ambayo hawakuyasema. Wanapaswa kujiepusha na malazimisho haya au kwamba mimi namkusudia huyu na yule katika ndugu zangu. Mwenye kuyadai hayo basi namshuhudisha Allaah ya kuwa ni mwongo. Haijalishi kitu ni nani. Kuna watu wanaowinda kwenye maji ya matope, kama alivosema Shaykh wetu Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) wakati walipoyafasiri maneno yake kimakosa. Alisema kuwa ambaye anasema kuwa nimemkusudia fulani na fulani au wanazuoni wa Madiynah wanawinda kwenye maji ya mapote.

Mwenye kusema kuwa nimemkusudia yeyote katika wanazuoni wetu kama vile  Shaykh Rabiy´, Shaykh ´Aliy bin Naasir, Shaykh Swaalih al-Fawzaan, Shaykh ´Abdul-Muhsin al-´Abbaad, Shaykh Swaalih al-Luhaydaan, Shaykh na Muftiy ´Abdul-´Aziyz Aal ash-Shaykh au wanafunzi wanaofuata mfumo wao ni mwongo mbaya. Nitamshtaki Siku ambayo haitofaa mali wala watoto isipokuwa ambaye atamjilia Allaah akiwa na moyo uliyosalimika. Hawakutosheka na ghushi hii. Bali wanasema eti mimi nimeyarekodi maneno tarehe 23 Ramadhaan. Sikuyarekodi tarehe 23 Ramadhaan, bali ilikuwa katika Sha´baan. Ilikuwa ni nasaha kwa ndugu zangu Salafiyyuun. Sikumlenga mtu yeyote. Ilikuwa ni nasaha kwa ndugu zetu Salafiyyuun na kila ambaye anaweka malazimisho au anavuka mipaka yake katika malazimisho yake. Aidha zilikuwa nasaha za jumla na zinawaelekea ndugu zangu wote Salafiyyuun na kila ambaye anavuka mipaka yake. Hata hivyo si sahihi kuwa nimemkusudia mtu maalum katika ndugu zetu. Wapo vijana wanaowafanyia vibaya ndugu, wanazuoni wa Salafiyyuun na ambao wanawanukuu kimakosa. Wanawawekea ndugu zao malazimisho yasiyotakikana. Tunalazimika kujihadhari na watu hao. Nimewaambia waalimu zangu na wanafunzi kujihadhari na wasumbuaji hawa ambao wanawinda kwenye maji machafu. Kuna uwezekano wakawa ni Hizbiyyuun waliyopenyezwa kati yetu. Tunapaswa kujihadhari nao. Inasikitisha jambo hili ni baya. Kuhusu nukuu hii na ambaye anasema kuwa nimemkusudia yeyote katika waalimu zetu nakariri kusema kuwa ni mwongo mbaya. Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

وَلاَ تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْؤُولاً

“Na wala usiyafuate yale usiyokuwa nayo elimu. Hakika masikio na macho na moyo, vyote hivyo vitaulizwa.”[2]

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hatamki yeyote neno isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha kuandika.”[3]

Tumcheni Allaah juu ya jambo hili. Tujitahidi kuzungumza ukweli na ya sawa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ

“Enyi walioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote, basi pelelezeni msije mkawasibu watu kwa ujinga, mkawa kuwa wenye kujuta juu ya ambayo mmeyafanya.”[4]

Tovuti yoyote inayonakili kutoka kwangu yasiyokuwa maneno haya na kuyaeneza ili kutumia fursa maneno yangu au maneno ya Shaykh mwingine yeyote ni yenye kutia shaka. Haijalishi kitu inajiita kuwa ni tovuti ya Sunnah na kadhalika. Hatuhadaiki kwa majina. Kadhalika ikiwa wanajiita “Kull Salafiyyiyn”, “al-Athariy” au majina mengine. Majina haya hayana maana yoyote.

[1] 16:125

[2] 17:36

[3] 50:18

[4] 49:06

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin Sa´d as-Suhaymiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=Qv87s76FeVA
  • Imechapishwa: 14/08/2023