10. Malipo ya subira kwa sababu ya kupoteza mtoto

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allalah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia kundi la wanawake wa ki-Answaar:

“Hakuna mmoja katika nyinyi atakayefisha watoto watatu ambapo akataraji malipo juu yao, isipokuwa ataingia Peponi.” Mwanamke mmoja katika wao akasema: “Vipi kuhusu wawili, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Na wawili.”[1]

  Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mwanamke mmoja alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Wanamme wameondoka kwa maneno yako. Tufanyie na sisi siku moja tukujie, ili utufunze katika yale aliyokufunza Allaah?” Akasema: “Kusanyikeni siku fulani na fulani.” Wakakusanyika na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaendea. Akawafunza katika yale aliyofunzwa na Allaah kisha akasema: “Hakuna kati yenu mwanamke mbaye atafisha watoto wake watatu, isipokuwa watakuwa ni kinga dhidi ya Moto.” Mwanamke mmoja akasema: “Vipi kuhusu wawili?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Na wawili. Na wawili. Na wawili.”[2]

Ameipokea an-Nasaa´iy.

Abu ´Ubaydah bin ´Abdillaah bin Mas´uud amesimulia kutoka kwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefisha watoto watatu katika miaka ya utoto, watakuwa kwake ni ngao madhubuti.” Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Nimepoteza watoto wawili.” Akasema: “Na wawili.” Ubayy bin Ka´b, bwana wa wasomaji, akasema: “Nimepoteza mmoja.” Akasema: “Na mmoja. Lakini hilo linahusiana na lile pigo la mwanzo.”[3]

Ameipokea Ahmad, Ibn Maajah na at-Tirmidhiy.

Imesihi ya kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Sina malipo ya kumpa mja Wangu muumini wakati ninapomchukua kipenzi chake wa duniani kisha akataraji thawabu, isipokuwa Pepo.”[4]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule ambaye atakuwa na watangulizi wawili[5], kutoka katika ummah wangu, basi Allaah atamwingiza Peponi kupitia wao.” ´Aaishah akasema: “Na yule mwenye mtangulizi mmoja kutoka katika ummah wako?” Akasema: “Pia yule mwenye mtangulizi mmoja, ee uliyewafikishwa.” Akasema: “Na yule asiyekuwa na mtangulizi kutoka katika ummah wako?”Akasema: “Mimi ni mtangulizi wa ummah wangu. Hawatofikwa na mfano wa yaliyonifika.”[6]

Ameipokea at-Tirmidhiy, Ahmad na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr”. 

Katika “Kitaab-ul-´Azaa’” Ibn Abiyd-Dunyaa amepokea kupitia kwa Dhwamrah bin Rabiy´ah, kutoka kwa Rajaa’ bin Jumayl al-Ayliy, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Yule mwenye kufa na hakumpoteza mtangulizi, basi hatofika Peponi isipokuwa kama mahali pa maji pasi na kuyanywa kikamilifu.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini mtangulizi?” Akasema: “Ni mtoto au mjukuu na ndugu mwema ambaye amejenga naye udugu kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Asiyekuwa na mtangulizi, basi mimi ni mtangulizi wake.”[7]

Kufika mahali pa maji pasi na kuyanywa kikamilifu ni ibara inayotumiwa kuonyesha uchache.

[1] Muslim (2632).

[2] al-Bukhaariy (10), (1249) na (7310) na Muslim (2633).

[3] at-Tirmidhiy (1061), aliyesema kuwa ni ngeni, Ibn Maajah (1606) na Ahmad (5/188). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (1061).

[4] al-Bukhaariy (6424).

[5] ´Aliy al-Qaariy amesema:

”Bi maana mtoto aliyekufa kabla mmoja katika wazazi wake. Mtoto huyo atawatayarishia maeneo pao Peponi.” (Jam´-ul-Wasaa-il (2/223))

[6] at-Tirmidhiy (1062), ambaye amesema kuwa ni nzuri na Swahiyh, na Ahmad (5/39-40). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (1062).

[7] Ahmad (5/83), Ibn Abiy ´Aaswim katika “al-Aahaad” (3303) na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (708). Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “Tajriyd Asmaa’-is-Swahaabah” (2/267).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 56-61
  • Imechapishwa: 14/08/2023