Katika ile Hadiyth ndefu ´Abdur-Rahmaan bin Samurah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Jana nimeona ndoto ya ajabu… Na nimemuona mtu, kutoka katika ummah wangu, ambaye mizani yake imekuwa khafifu. Ndipo wakaja watoto wake, waliokuwa kabla ya kubaleghe, na ndipo mizani yake ikawa nzito.”[1]

Khallaad bin Mansuur al-Waasitwiy amesema: Daawuud bin Abiy Hind ametuhadithia:

”Nimeona usingizini kama kwamba Qiyaamah kimetokea na kana kwamba watu wanaitwa katika hesabu. Nikapelekwa kwenye mizani. Matendo yangu mema yakawekwa kwenye sahani moja na matendo yangu maovu katika sahani jingine, ambapo maovu yangu yakashinda uzito matendo yangu mema. Nilipokuwa katika hali hiyo mwenye huzuni, nikapewa kitu kama leso au kitambaa cheupe ambacho kikawekwa pamoja na matendo yangu mema, kwa hivyo yakawa na uzito zaidi. Akaambiwa: ”Unajua ni kitu gani hiki?” Nikasema: ”Hapana.” Ni mimba yako iliyoharibika.” Nikasema: ”Nilikuwa na msichana wangu mdogo aliyefariki.” Nikaambiwa: ”Huyo si wako, kwa sababu ulikuwa ukitamani afe.”

Daawuud bin Abiy Hind alimuona Anas bin Maalik. Alikuwa ni mmoja katika watu vigogo wa ummah, mwenye kufunga siku zote na mwenye kumtii Allaah. Alifariki mwaka wa 140.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu ambaye atafisha watoto watatu akaingia Motoni, isipokuwa utamgusa kidogo.”

”Hakuna muislamu yeyote atayefisha watoto watatu aguswe na Moto, isipokuwa ni kwa lengo tu la kutekeleza kiapo.”[2]

Ameipokea at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy. at-Tirmidhiy amesema:

”Vivyo hivyo ameisimulia ´Umar, Mu´aadh, Ka´b bin Maalik, ´Utbah bin ´Abd, Umm Sulaym, Jaabir, Anas, Abu Dharr, Ibn Mas´uud, Abu Tha´labah al-Ashja´iy, Ibn ´Abbaas, ´Uqbah bin ´Aamir, Abu Sa´iyd na Qurrah bin Iyaas al-Muzaniy (Radhiya Allaahu ´anhum).”

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

”Mwanamke mmoja alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa na mtoto wake wa kiume akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Muombee du´aa. Hakika nimekwishazika watatu.” Akasema: “Umeshazika watatu?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema: “Hakika umejichukulia kinga madhubuti kutokana na Moto.”[3]

´Aliy bin ´Ayyaash amesema: Hafsw ametuhadithia: ´Aaswim ametuhadithia, kutoka kwa Abu Raziyn, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allâhu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna waislamu wawili ambao wanafisha watoto watatu, isipokuwa watakuwa ni ukuta kati yao na Moto.”

´Utbah bin ´Abd as-Sulamiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakuna mwanamme ambaye atafisha watoto watatu miaka ya utoto, isipokuwa watampokea katika milango minane ya Peponi; ataingia kupitia mlango anaoutaka.”[4]

Ameipokea Ibn Maajah na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr”.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna waislamu wawili ambao watafisha watoto watatu katika miaka ya utoto, isipokuwa Allaah atawaingiza wao na wazazi wao Peponi. Watasimama katika mlango miongoni mwa milango ya Peponi, ambapo waambiwe: “Ingieni Peponi!” Ndipo waseme: “Mpaka kwanza waje wazazi wetu.” Wataambiwa hivo mara tatu ambapo watajibu vivyo hivyo. Ndipo wataambiwa: “Ingieni Peponi nyinyi na wazazi wetu kutokana na fadhilah za huruma ya Allaah.”[5]

[1] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (2086).

[2] al-Bukhaariy (1251) na (6656), Muslim (2632), Ahmad (7264), at-Tirmidhiy (1060), an-Nasaa’iy (4/25) na Ibn Maajah (1603).

[3] Muslim (2636).

[4] Ibn Maajah (1604) na at-Twabaraaniy (17/119) na (17/125). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (1313).

[5] an-Nasaa’iy (4/25) na Abu Ya´laa (6079).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 50-55
  • Imechapishwa: 14/08/2023