11 – Sahl bin Sa´d as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waja hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth hii ni dalili juu ya adabu wapo miongoni mwa adabu za futari; nayo ni kuharakisha pindi unapofika wakati wake. Maana ya kuharakisha kukata swawm ni pale tu itapopotea diski ya jua kwenye upeo wa macho. Kufanya hivo ni kheri kubwa. Jengine ni kufata mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutendea kazi Sunnah yake. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiharakisha kukata swawm. ´Abdullaah bin Abiy Awfaa (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika moja ya safari ilihali amefunga. Wakati jua lilipozama akawaambia baadhi ya watu: “Tuchangie shayiri ya unga na maji.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Laiti ungelijizuilia kidogo.” Akasema tena: “Shuka chini utuchangie shayiri ya unga na maji.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Laiti ungelijizuilia kidogo.” Akasema tena: “Shuka chini utuchangie shayiri ya unga na maji.” Akasema: “Bado uko ni mchana.” Akasema tena: “Shuka chini utuchangie shayiri ya unga na maji.” Akashuka chini na akawachangia shayiri ya unga na maji ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanywa kisha akasema:

“Mkiona usiku umekuja hapa basi amekwishafungua mfungaji.”[2]

Imepokelewa kwamba kuharakisha kukata funga ni miongoni mwa tabia za Mitume. Hivo ndivo alivosema Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh):

“Sifa tatu ni miongoni mwa tabia za Mitume: kuharakisha kukata swawm, kuchelewesha daku na kuweka mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto ndani ya swalah.”[3]

Kuharakisha kukata funga ni kuwafanyia wepesi watu na ni kujiweka mbali na sifa ya kuchupa na kupindukia mpaka katika dini. Adabu hii waliitendea kazi watu wa karne bora ambao ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Abu Sa´iyd al-Khudriy alikata swawm wakati ilipozama diski ya jua.”[4]

´Amr bin Maymuun al-Awdiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa ni watu wanaoharakia zaidi kukata swawm na wenye kuchelewesha zaidi daku.”[5]

Ambaye atakata swawm hali ya kudhani kuwa jua limekwishazama ilihali bado halijazama, basi funga yake ni sahihi. Ni mwenye kupewa udhuru. Lakini anatakiwa kujizuilia na chakula mpaka lizame. Kwa sababu ni kama ambaye amekula kwa kusahau. Msahaulifu na mwenye kukosea hukumu zao ni moja. Amesema (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[6]

Mfungaji anatakiwa atumie fursa ya nyakati za kukata swawm na nyakati za kuitikiwa du´aa na aombe yale mambo ya kheri anayopenda. Kwani hakika du´aa za mfungaji ni zenye kuitikiwa. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu hazirudishwi nyuma du´aa zao; kiongozi mwadilifu, mfungaji wakati anapokata swawm na du´aa ya aliyedhulumiwa.”[7]

´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mfungaji wakati wa kukata swawm yake anayo du´aa isiyorudishwa nyuma.”

Ibn Abiy Mulaykah amesema:

“Nimemsikia ´Abdullaah bin ´Amr akisema wakati anapokata swawm:

اللهم إني أسألك برحمتك التي وسعت كلّ شيء أن تغفر لي

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa rehema Zako zilizokienea kila kitu unisamehe.”[8]

Miongoni vilevile mwa mambo yanayopendeza kusema wakati wa kukata kwake swawm ni yale aliyopokea ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema wakati wa kukata kwake swawm:

ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتِ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الْأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ

“Kiu kimeondoka, mishipa imerowana na ujira umepatikana – Allaah akitaka.”[9]

Ee Allaah! Turuzuku elimu yenye manufaa, matendo yenye kukubaliwa na riziki halali. Ee Allaah! Tuitikie du´aa zetu, tuhakikishie matarajio yetu, tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1957) na Muslim (1098).

[2] al-Bukhaariy (1954) na Muslim (1101).

[3] at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr” kama ilivyo katika “Majma´-uz-Zawaaid” (02/105) na akasema:

”…. imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Abud-Dardaa´. Ni Swahiyh kutoka kwa Swahabah. Ambayo inatoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wapo wapokezi ambao sipati ambaye amewaandikia wasifu wao.”

[4] Fath-ul-Baariy (04/196).

[5] ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (04/226). Amesema katika ”Fath-ul-Baariy” (04/199):

”cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

[6] 02:286

[7] at-Tirmidhiy (3598) na Ibn Maajah (1752). Hadiyth hii iko na nyenginezo zinazoitia nguvu kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[8] Ibn Maajah (1753), al-Haakim (01/422) na Ibn-us-Sunniy (481). al-Buuswiyriy amesema:

“Cheni hii ni Swahiyh.”

Tazama “az-Zawaaid”, uk. 254. Kuna walakini katika kuisahihisha kwake. al-Mundhiriy ameidhoofisha katika ”at-Targhiyb” (02/89). Hadiyth zilizopokelewa kuhusu maudhui haya hazisalimiki kutokamana na kutiliwa kasoro. Lakini pengine baadhi yake zikatia nguvu nyengine. Ukiongezea yale mapokezi kuhusu maudhui haya kutoka kwa Salaf. Tazama “Tafsiyr Ibn Kathiyr” (02/66-67) na “Tanbiyh-ul-Qaariy´” (78-79) ya Shaykh ´Abdullaah ad-Duwaysh (Rahimahu Allaah) na “Zawaaid-us-Sunan al-Arba´ah ´alaas-Swahiyhayn fiy Kitaab-is-Swiyaam” (01/239).

[9] Abu Daawuud (2357), al-Bayhaqiy (04/239), al-Haakim (01/422), Ibn-us-Sunniy (478) na ad-Daaraqutwniy (02/185) ambaye amesema:

“Ameipokea al-Husayn bin Waaqid peke yake. Cheni ya wapekezi wake ni nzuri.”

Huyu al-Husayn ni mwaminifu (ثقة) lakini anakosea, kama ilivyo katika ”at-Taqriyb”.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 33-31
  • Imechapishwa: 24/04/2022