10 – Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuleni daku. Kwani daku ina baraka.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth ni dalili inayoonyesha kuwa mfungaji ameamrishwa kula daku. Ndani yake mna kheri nyingi na baraka kubwa za kidini na kidunia. Kutaja kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baraka ni kwa minajili ya kuikokoteza na kuihimiza.

Daku ni kile kinacholiwa katika wakati wa mwisho wa usiku.

Amri hii iliyotajwa katika Hadiyth ni amri ya mapendekezo na sio amri ya ulazima kwa maafikiano. Dalili ya hilo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi kuunganisha swawm na Maswahabah zake pia wakafanya hivo pamoja naye. Kuunganisha (الوصال) ni mtu kufunga siku zisizopungua mbili na wala asifungue. Bali akafunga mchana na usiku wake.

Daku ina baraka kubwa zinazokusanya manufaa ya duniani na Aakhirah:

1 – Miongoni mwa baraka za daku ni kumpa mtu nguvu za kufanya ´ibaadah, kujisaidia kumtii Allaah katika kipindi cha mchana ikiwa ni pamoja na swalah, kusoma Qur-aan na kumtaja Allaah. Mwenye kuhisi nja anahisi uvivu wa kufanya ´ibaadah kama ambavo anahisi uvivu wa matendo yake ya kila siku. Hili ni jambo lenye kuhisiwa.

2 – Miongoni mwa baraka za daku inamfanya mlaji daku kuzidisha swawm kwa sababu ya ule wepesi kutokana na ile daku. Matokeo yake akawa na shauku ya kufunga na wala asihisi dhiki.

3 – Miongoni mwa baraka za daku ni kufata Sunnah. Mlaji daku akinuia kwa daku yake kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuiga kitendo chake, basi daku yake inakuwa ´ibaadah na hivyo anapata ujira kwa nia hii. Mfungaji akinuia kwa kula na kunywa kwake kuutia nguvu mwili wake juu ya swawm na kusimama usiku, basi analipwa thawabu kwa hilo pia.

4 – Miongoni mwa baraka za daku ni kwamba mtu anasimama mwishoni mwa usiku kufanya Dhikr, kuomba du´aa na kuswali. Kipindi hicho kuna uwezekano mkubwa wa mtu kuitikiwa.

5 – Miongoni mwa baraka za daku ni kwamba kuna kwenda kinyume na mayahudi na manaswara. Muislamu anatakiwa kujieka mbali na kujifananisha nao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kipambanuo kati ya funga yetu na funga ya Ahl-ul-Kitaab ni kula daku.”[2]

6 – Miongoni mwa baraka za daku ni mtu kuswali Fajr na mkusanyiko katika ule wakati wake wenye ubora. Kwa ajili hii utaona kuwa waswaliji ndani ya Ramadhaan wanakuwa wengi zaidi ukilinganisha na miezi mingine. Kwa sababu wameamka kwa ajili ya daku.

Daku inapatikana kwa kile kichache anachotumia mtu katika vyakula au vinywaji. Daku haihusiani na chakula maalum. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Neema ya daku ya muumini ni tende.”[3]

Miongoni mwa adabu za swawm ni mfungaji asifanye ubadhirifu katika chakula cha daku kwa njia ya kwamba akajaza tumbo lake kwa chakula. Bali anatakiwa kula kwa kiwango. Mwandamu hajapatapo kujaza chombo kiovu zaidi kama tumbo. Pale anaposhiba wakati wa daku hatonufaika na wakati wake mpaka karibu na Dhuhr. Wingi wa kula unapelekea katika uvivu na uzembe. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Neema ya daku ya muumini ni tende.”

kunaashiriwa maana hii. Tende, ukiongezea thamani yake ilioko juu ya lishe, ni nyepesi tumboni na rahisi kusagwa. Ukimlinganisha na ambaye ameshiba hukesha usiku na akalala mchana. Amekosa malengo ya swawm. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.

Ee Allaah! Hakika sisi tunakuomba kheri zote tunazozijua na tusizozijua, tulinde na shari zote tunazozijua na tusizozijua, tuepushe na maadili, matendo na matamanio mabaya. Tusamehe ssi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1923) na Muslim (1095).

[2] Muslim (1096).

[3] Abu Daawuud (2345), Ibn Hibbaan (08/253) na al-Bayhaqiy (04/236). Ndani yake kuna Muhammad bin Muusa al-Fitwriy ambaye ametiwa dosari. Kuna kundi la maimamu ambao wamemfanya kuwa mwaminifu. Haafidhw amesema katika ”at-Taqriyb”:

”Ni mkweli. Lakini ametuhumiwa Tashayyu´.”

Maana ya Hadiyth hii imekuja kutoka kwa kundi la Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 30-32
  • Imechapishwa: 24/04/2022