07. Kuchelewesha deni la Ramadhaan mpaka Ramadhaan nyingine

Haijuzu kwa mtu kuchelewesha kulipa siku anazodaiwa za Ramadhaan mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine. Kwani ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amefanya Ramadhaan ndio kikomo. Akichelewesha kutokana na udhuru kwa njia ya kwamba kushindwa kwake kukakutana na maradhi, safari na mfano wa hayo na asiweze kulipa mpaka akaingiliwa na Ramadhaan nyingine, basi hakuna dhambi juu yake. Amesema (Ta´ala):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

Kwa hivyo atalipa siku anazodaiwa baada ya kumalizika Ramadhaan ya sasa.

Akizembea na akachelewesha kulipa pasi na udhuru mpaka akaingiliwa na Ramadhaan nyingine, basi atafunga baada ya Ramadhaan ya sasa na halazimiki kulisha chakula. Hilo ni kutokana na udhahiri wa maneno Yake (Ta´ala):

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“… hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[2]

Hata hivyo atalazimika kutubu na kuomba msamaha kutokana na upungufu huu. Ijapo kuna baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), akiwemo Ibn ´Abbaas na Abu Hurayrah, ambao wametoa fatwa ya kwamba mtu huyo anatakiwa kumlisha chakula masikini kwa kila siku moja aliyochelewesha pamoja na kulipa swawm. Pengine waliona hivo kutokana na Ijtihaad na kumtia adabu mzembeaji huyu na kufidia upungufu huu kwa kumuwajibishia kulisha chakula.

ad-Daaraquwniy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhum) kuhusu ambaye amezembea katika kulipa deni la Ramadhaan mpaka akaingiliwa na Ramadhaan nyingine ambapo akasema:

“Huyu afunge pamoja na wengine na afunge ile Ramadhaan aliyozembea na alishe chakula kwa kila siku iliyompita kumpa masikini.”[3]

Yamepokelewa mfano wa haya kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Kutendea kazi fatwa hii kuna mashiko ingawa ni kwa njia ya mapendekezo[4]. Kwa sababu aina hii ni katika kuziba upungufu kwa njia ya kutoa swadaqah na swadaqah imependezeshwa kwa ujumla. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] 02:286

[2] 02:184

[3] ad-Daaraqutwniy (02/197) ambaye amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

Vivyo hivyo yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh (02/197).

[4] Ambaye anaona kuwa maoni ya Swahabah sio hoja anaweza kutendea kazi maoni haya ijapo ni kwa njia ya mapendekezo. Kuhusu ulazima hakukuthibiti kitu kilichorufaishwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah ndiye mjuzi zaidi. 

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 13/03/2023