08. Maiti aliyekufa akiwa na deni la swawm ya wajibu

04 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye atakufa na anadaiwa swawm, basi atafungiwa na walii wake.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha kuwa ambaye amekufa na huku anadaiwa swawm ya lazima basi inapendeza kwa walii, ambaye ni nduguye, kumfungia swawm hiyo. Kufanya hivo ni kumtendea wema, kuunga kizazi na kunatakasa dhimma yake  – Allaah akitaka. Makusudio ya walii ni wale warithi wake au jamaa zake. Warithi ndio ndugu walio karibu zaidi.

Hadiyth ni yenye kuenea juu ya kila swawm ambayo ni lazima kwa maiti. Ni mamoja ni lazima kwa mujibu wa Shari´ah, kama vile swawm ya Ramadhaan, au ni lazima kwa kuweka nadhiri kwa mujibu wa moja kati ya maoni mawili. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Mwanamke mmoja alikuja kwa Mtume wa Allaah ambapo akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amefariki na anadaiwa swawm ya nadhiri. Je, nimfungie?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, unaonaje iwapo mama yako angelikuwa na deni ambapo ukamlipia si ungelikuwa umelilipa kwa niaba yake?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Mfungie mama yako.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na anadaiwa swawm ya mwezi. Je, nimfungie?” Akamuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Mama yako angelikuwa na deni si ungemfungia?” Akasema: “Ndio.” Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Deni la Allaah lina haki zaidi kulipwa.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Dada yangu amefariki… “[2]

Mapokezi yote haya yanatoa faida kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa juu ya swawm ya nadhiri na aliulizwa swawm ya mwezi. Kuna uwezekano ikawa ni Ramadhaan au ikawa nadhiri. Katika zote hizo amesema:

“Deni la Allaah lina haki zaidi kulipwa.”

Zinafahamisha haikuwa tukio moja. Faida nyingine tunayopata ni kwamba Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ni miongoni mwa kanuni zilizoenea ambazo zimefahamishwa na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na kwamba inahusu kila funga ambayo imemlazimu maiti na akaweza kuifunga katika uhai wake lakini hata hivyo asifanye hivo. Haya ni matukio mbalimbali na kila mmoja aliuliza kutokana na hali iliyomtokea. Hata hivyo matukio yote jawabu limekuja kwa njia ya amri ya kulipa. an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maoni sahihi ni kufaa kihakika kabisa kumfungia maiti. Ni mamoja swawm hiyo ni ya Ramadhaan, swawm ya nadhiri na swawm nyenginezo za wajibu. Hilo ni kutokana na Hadiyth ambazo ni Swahiyh na hazina vipingamizi.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[2] Hadiyth ya Ibn ´Abbaas katika al-Bukhaariy (1953), Muslim (1148) na ”Fath-ul-Baariy” (04/194) na ukaguzi wa Ahmad Shaakir wa ”al-Musnad” nr. (3420).

[3] al-Majmuu´ (06/370). Tazama ”Sharh-un-Nawawiy ´alaa Swahiyh Muslim” nr. (1147-11480).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 15/03/2023