05. Wataokuwa na njaaa sana siku ya Qiyaamah

19 – ´Abdul-´Aziyz bin Yahyaa ametuhadithia: ´Aliy bin Thaabit al-Jazariy ametuhadithia, kutoka kwa al-Waliyd bin ´Amr bin Saaj, kutoka kwa ´Awn bin Abiy Juhayfah, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Nilikula mkate wa ngano na nyama ya mafuta na baadaye nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoa bweu. Akasema: ”Acha kutoa bweu. Hakika wanaoshiba zaidi katika nyinyi ndio wataokuwa na njaa zaidi siku ya Qiyaamah.” Kuanzia siku hiyo Abu Juhayfah hajapatapo kula akalishibisha tumbo lake mpaka alipoiacha dunia.”

20 – Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia: Mu´aadh bin Hishaam ametukhabarisha: Baba yangu amenihadithia, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Anas bin Maalik, ambaye amesema:

”Nilitembea kwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikiwa na mkate wa shayiri na mafuta yaliyoyeyuka ambayo yamebadilka kwa muda. Aliweka rehani ya ngao ya vita kwa myahudi na nilimsikia mara nyingi akisema: ”Naapa kwa Allaah! Familia ya Muhammad haikupambaukiwa ikiwa na pishi ya tende wala pishi nne ya nafaka.” Kipindi hicho alikuwa na wake wanne.”[1]

21 – Ishaaq ametuhadithia: Hajjaaj ametuhadithia, kutoka kwa Mubaarak, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Anas bin Maalik, ambaye amesema:

”Niliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye alikuwa amejiegemeza kwenye kitanda kilichofumwa kwa utepe. Hakukuwa na kitani cha kitanda kati ya ngozi yake na mkanda. Chini ya kichwa chake kulikuwa na mto wa ngozi uliojazwa nyuzi za mkuti. Maswahabah wengi wakamtembelea, lakini alipoingia ´Umar, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akageuka kwa haraka. Akatazama na kuona namna ambavyo mkanda umemuathiri kwenye ubavu wake. ´Umar akaanza kulia ambapo Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ni kipi kinachokuliza, ee ´Umar?” Akasema: ”Naapa kwa Allaah, ee Mtume wa Allaah! Hakuna kinachoniliza isipokuwa ni vile najua kuwa wewe ni mtukufu zaidi mbele ya Allaah kuliko Kisraa na Qayswara, ambao wanaishi katika yale wanayoishi katika dunia, ilihali wewe uko katika sehemu ninayoiona.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Je, hivi huridhii, ee ´Umar, ya kwamba wao wako na dunia na sisi tuko na Aakhirah?” Akasema: ”Ndio,  naapa kwa Allaah, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: ”Mambo ndio hivo.”

[1] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (1215).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 40-43
  • Imechapishwa: 11/06/2023